Serikali kupitia wizara ya afya imetangaza kutoa shilingi bilioni 9 kwa mamlaka ya afya SHA, katika harakati ya kulipa madeni yanayodaiwa na hospitali baada ya kutoa huduma chini ya bima ya kitaifa ya afya iliyotolewa NHIF.
Katibu katika wizara hiyo Harry Kimtai ametangaza kutolewa
kwa fedha hizo mapema Jumanne akiwa katika kaunti ya Nakuru wakati wa ufunguzi
wa kamati ya sekta mbali mbali katika jimbo ya bonde la ufa.
Kimtai amesema kuwa fedha hizo zitasambazwa kwa hospitali
kufikia mwisho wa wiki hii ikiwemo shilingi bilioni moja iliyotolewa kwa wakfu
wa Linda Mama kuwasaidia wanawake wajawazito kujifungua katika hospitali bila
malipo.
Katibu huyo pia amesisitiza haja ya wizara kutoa malipo kwa
hospitali kwa wakati unaostahili ili wagonjwa wanaotafuta huduma za afya katika
hospitali mbali mbali wapate huduma hiyo bila ya kufukuzwa wala kutoa fedha
mfukoni ili kutibiwa.
Wizara ya afya imetia sahihi kwa mikataba 26 na baraza la
magavana kuboresha vifaa vya matibabu katika hospitali za umma pamoja na
kuwatuma nyanjani maafisa 70 wa kiufundi katika vituo vya afya vya kaunti.
Mkutano wa Nakuru umewaleta pamoja maafisa wa kamati tendaji
za kaunti CEC kutoka kaunti za Nakuru, Uasin Gishu, West Pokot, Bomet, Kericho,
Nandi, Narok, Baringo, Samburu, Turkana, Laikipia na Nyandarua.
Kamati iliyozinduliwa imetwikwa jukumu la usajili wa
wananchi katika mamlaka mpya ya afya nchini SHA.
Katibu Harry Kimtai aidha amezitaka serikali za kaunti
kueneza injili ya SHA kwa wakaazi wa maeneo yao ili kuwezesha hatua za serikali
kuu kuafikia utoaji wa afya kwa kila mmoja.