Serikali ya Uganda imefichua kwamba ilishirikiana na mamlaka nchini Kenya kumkamata kiongozi wa upinzani Kizza Besigye.
Waziri wa ICT na Mwongozo wa Kitaifa wa Uganda Chris Baryomunsi amesema serikali ya Kenya ilifahamu na ilishiriki katika kukamatwa kwa kiongozi wa upinzani Kizza Besigye jijini Nairobi.
Matamshi ya waziri huyo wa Uganda yanakinzana na yale ya katibu wa kudumu wa mambo ya nje wa Kenya Dkt. Korir SingOei aliyesema kuwa mamlaka nchini Kenya haikufahamu au kushiriki katika kutiwa mbaroni na kisha kusafirishwa Uganda kwa Besigye.
Akizungumza Ijumaa, Novemba 22, waziri huyo Chris Baryomunsi alisema Serikali ya Uganda ilikuwa inawasiliana na serikali ya Kenya kabla ya kukamatwa kwa Besigye. Baryomunsi alisema kuwa haingewezekana kumkamata na kumsafirisha Besigye hadi Uganda kama mamlaka ya Kenya haikufahamu.
"Serikali ya Uganda ilikuwa inawasiliana na serikali ya Kenya, kama sivyo ungemkamataje mtu katikati ya Nairobi kisha kumrudisha Uganda kupitia uwanja wa ndege au hata kwa njia ya barabara bila ufahamu kamili na msaada wa serikali," alisema katika mahojiano na Televisheni ya NBS.
Besigye alikuwa nchini Kenya kwa ajili ya uzinduzi wa kitabu cha Martha Karua kabla ya kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi kwa nguvu na kusafirishwa hadi jela ya kijeshi mjini Kampala. Kulingana na Martha Karua, mwanasiasa huyo alikuwa amefika Nairobi siku ya Jumamosi, Novemba 16, na kuingia katika Hoteli ya Waridi Paradise and Suites.
Besigye kisha aliondoka hotelini na dereva wa teksi kwa mkutano katika 108 Riverside Apartments na hapo ndipo alitoweka. Besigye alikuwa amepangiwa kuhudhuria na hata kuhutubia mkutano wa uzinduzi wa kitabu cha Martha Karua siku ya Jumapili Novemba 17, lakini alitiwa mbaroni kabla ya siku hiyo.