Maafisa wa upelelezi kutoka kaunti ndogo ya Sotik wanamtafuta afisa mmoja wa polisi anayesemekana kuwa OCS katika kituo kimoja cha polisi katika Kaunti ya Trans Zoia kwa kumpiga risasi mkaazi wa eneo la Sotik kwa jina Charles Mutai tumboni mwendo wa saa saba usiku wa Jumanne katika kisa kilichotokea katika sehemu moja ya burudani iliyoko Kapcherany.
Kisa hicho kinadaiwa kutokea wakati afisa huyo alikuwa katika likizo fupi nyumbani ila kiini cha kumpelekea kumfyatulia mwathiriwarisasi hakijajulikana.
Kufuatia kupigwa risasi, Mutai alikimbizwa katika hospitali ya Kapkatet kwa huduma ya kwanza kabla ya kuhamishiwa katika Hospitali ya Misheni ya Litein kwa matibabu zaidi. Kwa mujibu wa polisi, mwathiriwa anaendelea kupokea matibabu na sasa amepata nafuu angalau.
Maafisa wa upelelezi waliotembelea eneo la uhalifu walipata mabaki ya risasi ya milimita 9 iliyotumika ambayo itakuwa muhimu katika uchunguzi wao.
Maafisa
wanaoendesha uchunguzi huo wamemtaka mshukiwa kujisalimisha mwenyewe ili kuhojiwa
kubaini sababu iliyopelekea kumpiga mwathiriwa risasi.