Familia ya wakili Willy Mutubwa imesema kuwa mpendwa wao aliaga kutokana na damu kuganda kwenye mapafu yake baada ya uchunguzi wa maiti uliofanywa kubaini hivyo.
Willy Mutubwa aliyekuwa naibu mwenyekiti wa mahakama ya migorogoro ya kisiasa nchini alizirai na kufa wakati akiwa kwenye kipindi cha mapumziko akihudhuria kikao cha mahakama mtandaoni jijini Nairobi mnamo Jumanne jioni.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa familia, ijapokuwa haijabainishwa kisayansia kuwa kuganda kwa damu ndiko kulisababisha kifo cha mwanasheria huyo, madaktari wanashuku kwamba damu kwenye mapafu ya Mutubwa kuganda kulisababishwa na jeraha ndogo alilolipata akicheza mpira wa magongo takribani mwezi mmoja uliopita.
Familia hata hivyo imekubali taarifa ya uchunguzi wa maiti kuwa sababu asili ya kifo cha ghafla cha Willy kilitokana na kuganda kwa damu kwenye mapafu yake.
Marehemu Willy Mutubwa atafanyiwa ibaada ya wafu mnamo Alhamisi, Desemba 5 katika kanisa la Consolata Shrine eneo la Wetslands jijini Nairobi kabla ya kusafirishwa nyumbani kwake ambako atazikwa Jumamosi Desemba 7. Ibaada ya mazishi itanyika katika shule ya Kakamega Approved.
Idara ya mahakama ikiongozwa na rais wake Jaji Mkuu Martha Koome, aliongoza wanasheria katika kutuma risala za rambi rambi kwa familia ya marehemu Willy Mutubwa akimtaja kuwa mtetezi mashuhuri katika utoaji wa haki nchini.
Vile vile chama cha wanasheria nchini LSK chini ya rais
Faith Odhiambo, kilimwomboleza Willy kikimtaja kuwa msomi na bingwa wa kutatua mizozo
nje ya mfumo wa mahakama maarufu kama Alternative Dispute Resolution ADR.