Mvua ambayo imekuwa ikinyesha katika maeneo mbali mbali ya nchi imesababa vifo vya zaidi ya watu 12 na kuacha zaidi ya familia 3,970 bila makao.
Katibu wa kudumu wa Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa, Dkt. Raymond Omollo amekuwa katika ziara ya kukagua athari za mafuriko. Siku ya Jumanne alikagua maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko katika kaunti za Busia na Kisumu ili kutathmini kiwango cha uharibifu, kusimamia usambazaji wa misaada, na kuwasiliana na familia zilizoathirika.
Katika Kaunti Ndogo ya Bunyala, Dkt. Omollo alitembelea Shule ya Msingi ya Lunyofu, ambayo kwa sasa inahifadhi familia 500 zilizohamishwa. Alisimamia usambazaji wa chakula na bidhaa zisizo za chakula, ikiwa ni pamoja na mchele, maharagwe, blanketi, na vifaa vya matibabu, akisisitiza dhamira ya serikali kwa usalama na kuokoa familia zilizoathirika. Akikiri kwamba zaidi ya familia 3,000 huko Busia zimeathiriwa na mafuriko, PS Omollo alisisitiza haja ya makazi endelevu katika maeneo salama.
Pia alitangaza mipango ya uendelezaji wa miundombinu, ikiwa ni pamoja na upanuzi wa lamba (dykes) na ujenzi wa bwawa la juu ya mto ambalo ni Kilomita 4-5 ili kudhibiti mtiririko wa maji na kusaidia unyunyiziaji mashamba maji na matumizi ya nyumbani.
“Wakati mvua zinatarajiwa kupungua hivi karibuni, lazima tuwe macho na kuzingatia maagizo ya usalama ya serikali. Hii ni pamoja na kuepuka maeneo hatari ikiwa ni pamoja na mabwawa, barabara na madaraja yanayochukuliwa kuwa si salama na kufuata notisi za kuhama,” alisema Dkt Omollo.
Katika Kaunti ya Kisumu, Katibu huyo wa kudumu pia alitembelea Kambi ya Watu Waliohama makwao ya Ogenya, inayo na familia 1,973. Omollo aliwataka wakazi wa Ogenya kushiriki katika Siku ya Chifu ya Utekelezaji wa Hali ya Hewa, inayofanyika kila Ijumaa ya kwanza ya mwezi, na kukumbatia mipango ya upandaji miti.
"Upanzi wa miti ni muhimu kwa kulinda mazingira yetu, kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, na kutatua changamoto za usalama wa chakula," alisema, akitoa wito wa umoja katika kukumbatia miradi ya maendeleo.
Omollo alipongeza mashirika mbalimbali ya kukabiliana na majanga, ikiwa ni pamoja na Kituo cha Kitaifa cha kushughulikia Mikasa na Msalaba Mwekundu, kwa hatua zao za haraka na zinazofaa.