KATIBU mkuu wa muungano wa wafanyikazi nchin, COTU,
Francis Atwoli ni wa hivi punde kurukia kauli ya ucheshi ya ‘…hiyo kitu
ikutoke’ ambayo imekuwa ikitumiwa kwa miktadha mbalimbali kwa wiki sasa.
Kupitia ukurasa wake wa X, Atwoli alitumia kauli hiyo
kumjibu mtumizi mmoja wa jukwaa hilo aliyetaka kujua ni lini atastaafu kutyoka
COTU.
“Bwana Atwoli, utastaafu lini? Mtumizi huyo kwa jina
Gideon Odinga alimuuliza.
Atwoli alisema kwamba yeye bado yuko kama mwakilishi
wa vyama vya wafanyikazi nchini, akisema kwamba ni vizuri jamaa huyo ameuliza
kwani swali hilo lilikuwa limemtatiza sana lakini baada ya kujikusanya kijasiri
na kuuliza, limemtoka.
“Uliza
tu hiyo swali hiyo kitu ikutoke…Niko hapa kuhudumia maslahi ya wanachama wa
vyama vya wafanyakazi,” Atwoli alisema.
Mzee huyo ambaye amekuwa usukani kama katibu wa COTU
kwa miaka kadhaa sasa alisema kwamba wadhifa wake hakuteuliwa bali yeye huwa
anachaguliwa na wanachama huku akifafanua kwamba watu wengi hawawezi elewa
jinsi vyama vya wafanyikazi hufanya kazi hadi pale watakapokuwa wanachama.
‘Sijateuliwa,
nachaguliwa na wanachama. Ukijiunga na muungano, utaelewa jukumu langu na la
COTU (K),’ Atwoli aliongeza.
Taaluma yake ilichukua mkondo wa kimataifa
alipochaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa COTU yenye nguvu mwaka 2001, nafasi ambayo
amechaguliwa kwa mihula mitano mfululizo.
Uchaguzi wa hivi punde ulifanyika katika Chuo cha
Wafanyakazi cha Tom Mboya huko Kisumu, ambapo mamia ya makatibu wakuu wa
muungano wa COTU walihudhuria, na angalau wengine 200 walihudhuria kwa njia ya
mtandao.
Katika hotuba yake ya kukubali kuchaguliwa tena,
Katibu Mkuu wa COTU (K) Francis Atwoli aliwashukuru wajumbe na wafanyikazi wa
Kenya kwa ujumla kwa kumwamini na majukumu mengine. Aliahidi kamwe hatasaliti
imani ambayo wafanyikazi wote wamempa kwa miaka iliyopita.