Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kwenye Radio Jambo, Joseph Ogidi almaarufu Gidi Ogidi, amemkumbuka marehemu Fidel Odinga miaka kumi baada ya kifo chake.
Wawili hao walikuwa marafiki wakubwa na mtangazaji huyo wa redio alipost moja ya picha zao wakiwa pamoja wakati wa kumsherehekea.
"Obange, bado unakumbukwa zaidi ya miaka 10 tangu kufariki kwako. Endelea kupumzika kwa amani,” Gidi aliandika.
Mtangazaji huyo wa kipindi cha asubuhi amekuwa akikumbuka na kuendelea kumsherehekea marehemu rafiki yake miaka baada ya kifo chake cha ghafla.
Marehemu Fidel alipatikana akiwa amefariki mnamo Januari 4, 2015 nyumbani kwake katika mtaa wa Karen, Nairobi baada ya tafrija ya usiku na marafiki. Alikuwa mwana mkubwa wa kiongozi wa chama cha ODM Raila Amollo Odinga.
Huku akimuomboleza baada ya kifo chake miaka kumi iliyopita, Gidi alionyesha jinsi alivyopatwa na taarifa za kusikitisha za kifo cha Fidel kwa mshtuko na kuitaka roho yake ipumzike kwa amani.
“Nimesikitishwa sana na taarifa za kufariki kwa rafiki yangu Fidel Odinga. Siamini kuwa ni miezi miwili tu iliyopita ambapo tulikuwa tukibarizi kwa furaha, tukiimba nyimbo za reggae na sasa umeenda. Roho yako ipumzike kwa amani ya milele Omuga! Inasikitisha sana,” Gidi alisema mnamoJanuari 2015.