POLISI katika kaunti ya Kisii wameanzisha uchunguzi kufuatia kisa cha kutamausha ambacho kilinaswa kwenye video mwanamume mmoja alimchapa viboko mwanamke kwa kudaiwa kuiba unga wa ngano.
Kwa mujibu wa ripoti, kisa hicho kilitokea katika Eneobunge
la Bomachoge Borabu ambapo mwanamke huyo alionekana akichaopwa viboko na mateke
na jirani yake, huku akiwa amempakata mwanawe mdogo mikononi.
Inaarifiwa kwamba jirani huyo alimshuku kwa kuiba
unga ngano wa kilo mbili kabla ya kuanza kumchapa.
William Kaibet, mkuu wa polisi Kenyenya alithibitisha
kupokea ripoti hiyo na kusema kwamba uchunguzi umeanzisha kumsaka mwanamume
aliyenaswa kwenye video hiyo akimshambulia mwanamke huyo.
“Hicho
kitendo ni lazima mtu awajibishwe mbele ya sheria. Na nadhani tukipata taarifa
zaidi tutawajulisha,” alisema.
Mwanamke huyo anatuhumiwa kwa kuchukua unga wa
shilingi 150 kutoka kwa nyumba ya mama mzee kabla ya kuanza kuchapwa bila
kupewa nafasi ya kujieleza.
Majirani wenzake walieleza kwamba anaishi na ulemavu
katika hali ya uchochole, jambo linalowafanya watu kumdharau.
“Hawa
watu walisimama hapa nje na huyu mzee alikuwa anamchapa akaniambia niingie kwa
nyumba nimwambie atoke nje aelezee kwa nini alipatikana nyumba ya mama akiiba
unga wa ngano. Hata nilihuzunika mimi sana kwa maana haya ni madharau kwa
sababu waliona hajiwezi ndio wamfanyie vibaya,”
jirani mmoja alieleza huku akitoa wito kwa njia ya kumsaidia huyo mwanamke
kupatikana.
Ni kisa ambacho kimezua gadhabu miongoni mwa wananchi
mitandaoni, huku wakitoa wito kwa mwanamume aliyenaswa kwenye video akimchapa
kuchukuliwa hatua za haraka kisheria.
Kudhalilishwa kwa mwanamke huyo kunajiri wakati
ambapo nchini Kenya kumeshuhudiwa jinamizi la unyanyasaji wa kijinsia na mauaji
dhidi ya wanawake, jambo ambalo mashirika mbalimbali ya kutetea haki za
binadamu yametoa wito kwa serikali kutafuta njia madhubuti kupata mwafaka wake
na kukomesha mauaji ya wanawake mikononi mwa wanaume na watu wa karibu.