WAKILI Danstan Omari ametangaza nia ya kuwania kiti cha useneta wa Nairobi 2027. Wakili huyo alisema kuwa Kaunti ya Nairobi inamhitaji akisema yeye ni mwaniaji thabiti wa nafasi hiyo.
Katika video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii
alasiri ya Jumatano, Omari alisema, "Nairobi inahitaji mtu imara kuwa
seneta; siasa za Nairobi ziko hivi; katika uchaguzi wa kwanza chini ya katiba
mpya 2013, Evans Kidero alikuwa gavana na Mike Sonko alikuwa seneta 2017, Sonko
alikua gavana huku Jonson Sakaja akiwa seneta 2022 Sakaja akawa gavana na Edwin
Sifuna akawa seneta.”
"Huu ni wakati wa Sifuna kuwa gavana, na kwa hivyo,
nitakuwa katika kinyang'anyiro cha kuchukua wadhifa wa Sifuna ili mwaka wa 2032,
niwe pia gavana wa Nairobi."
Wakili huyo alisema Nairobi ni jiji kubwa barani Afrika na
ndipo Rais anapoishi, na kuongeza kuwa linahitaji mtu thabiti, aliye makini na
aliye na wasifu.
Alisema kuwa atakuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa pesa
zinazotolewa jijini zinatumika ipasavyo kwa maendeleo ikiwa atanyakua kiti cha
useneta.
"Nataka kuingia kama Danstan Omari, ambaye amekuwa
kortini na kuwatetea wachuuzi, wapiga debe, waendesha bodaboda na jumuiya za
wafanyabiashara wanaoanza kutoka biashara ndogo zaidi ya Sh5 hadi rasilimali za
shilingi bilioni. Hiyo ndiyo sauti inayokosekana katika Seneti. ,"
aliongeza.
Wakili huyo aliongeza kuwa alianza kazi yake huko Nyamira,
akahamia Nairobi, na sasa ni mtu wa kimataifa.
"Iwapo nitasimama kama mgombea binafsi au kwenye chama
chochote, nitauza sera na nyadhifa zangu kama Danstan Omari," wakili huyo
aliongeza.
Wakili wa jiji amewawakilisha wateja mbalimbali katika kesi
kuanzia kusababisha fujo katika maandamano hadi mauaji.