KATIBU katika wizara ya usalama wa ndani Raymond Omollo amefichua kwamba maafisa wa polisi wa Kenya waliotumwa nchini Haiti wamepiga hatua kubwa katika kurudisha amani na utulivu mitaani katika jiji la Port-au-Prince.
Omollo alitoa taarifa
hizo kupitia ukurasa wake kwenye X alipochapisha klipu ya afisa mmoja wa Kenya
akiwaimbisha watoto darasani nyimbo za Kiswahili na tafsiri kwa Kifaransa.
Omollo alisema kwamba
kabla ya maafisa wa polisi wa Kenya kupelekwa nchini Haiti, mitaani kulikuwa na
machafuko ambayo yalifanya shughuli za masomo kuwa ngumu.
Wahalifu waliwachukua
watoto na kuwatumia kama vichocheo kwenye vita ambavyo vilizua taharuki
kimataifa.
“Polisi wa Kenya,
wanaoongoza ujumbe wa kulinda amani unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa nchini
Haiti, wamepata maendeleo ya ajabu katika kurejesha utulivu, hasa katika sekta
ya elimu.”
“Kwa miaka mingi,
unyanyasaji wa magenge ulikumba jamii, huku watoto wa umri wa kwenda shule mara
nyingi wakiandikishwa kama vichocheo katika migogoro hii, na kuwanyima elimu na
hali ya kawaida,” Omollo alichapisha.
Omollo alisisitiza kuwa
mafanikio ya misheni hiyo yanawakilisha hatua muhimu ya kuvunja mzunguko wa
vurugu na kutoa matumaini kwa vijana wa Haiti.
"Shule
zimefunguliwa tena, na watoto ambao hapo awali walinaswa katika vita vya
magenge sasa wamerudi madarasani, wakidai tena haki yao ya elimu na mustakabali
mwema.
"Hatua hii muhimu
inasisitiza mafanikio ya ujumbe wa kulinda amani katika kuvunja mzunguko wa
vurugu na kuendeleza matumaini kwa vijana wa Haiti, kuhakikisha kuwa
wameandaliwa kujenga taifa lao," Omollo
aliongeza.
Taarifa hii inafuatia
kutumwa hivi majuzi kwa maafisa 217 zaidi wa polisi wa Kenya nchini Haiti mnamo
Ijumaa, Januari 17, 2025.
Katibu wa Baraza la
Mawaziri Kipchumba Murkomen, PS Omollo, Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas
Kanja, na maafisa wengine wakuu walisimamia kutumwa.