MBUNGE wa Embakasi Mashariki Babu Owino ameonyesha sikitiko lake kwa wakaazi wa Nairobi na haswa watumizi wa barabara nyakati hizi za mvua nyingi.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook,
Babu Owino alichapisha picha ya mwendesha bodaboda mmoja aliyepigwa picha
akijaribu kuiokoa pikipiki yake kutoka dimbwi la maji barabarani.
Owino alisema kwamba ni sikitiko
kubwa kwa mwendesha bodaboda huyo kwani sasa huenda pikipiki yake imeharibika
injini kutokana na kuzama kwenye maji barabarani.
Mbunge huyo anayedaiwa kuwa mbioni
kujitosa katika kinyang’anyiro cha ugavana Nairobi alionekana kuulaumu uongozi
wa jiji akisema kwamba gavana Sakaja ameshindwa kazi.
Owino alisema kwamba Sakaja
ameshindwa kutatua suala la mabomba ya kupitisha maji chafu na kusababisha
mafuriko kushuhudiwa kwenye barabara nyingi za Nairobi pindi mvua zinaponyesha.
“Moyo wangu unauma ninapomuona
huyu mwendesha Bodaboda anayetegemea mashine hii kujipatia riziki; kulipia karo
ya shule kwa watoto wake, kununua chakula, kulipa karo ya kila mwezi na kulipia
gharama nyinginezo.”
“Mtu huyu anapata takriban
200/- tu kwa siku baada ya kununua mafuta lakini pikipiki yake haitafanya kazi
tena kwa sababu injini imezama ndani ya maji kutokana na mfumo mbovu wa
mifereji ya maji jijini Nairobi ambayo inaletwa na Uongozi duni kutoka kwa
Gavana asiye na uwezo.”
“Wengi wa waendesha Bodaboda
huchukua pikipiki hizi kwa mkopo na lazima walipe bila kujali hatari yoyote ya
kikazi inayowapata. Tuna jumla ya bajeti ya shilingi Bilioni 42 lakini Gavana
hafanyi lolote, ni mzuri tu kwa visingizio. Wanairobi wasimchague tena asiye mwanataaluma
katika Nafasi hii. #Nairobi inazama,” Owino
alisema.
Katika kipindi cha wiki moja, Nairobi
sawa tu na maeneo mengine nchini yamekuwa yakishuhudia mvua nyingi ambazo idara
ya utabiri wa hali ya hewa imesema kwamba mvua hizo zitakata kuanzia wikendi
hii.