logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Babu Owino Asimulia Kuzuiliwa Tanzania, Ataka Rais Suluhu Kumuomba Msamaha

“Nilikwenda Tanzania, Nilipowasilisha hati yangu ya kusafiria kwa ajili ya kibali cha uhamiaji waliandika, “Interpol Wanted List.” Niliwekwa kizuizini huko kwa saa tatu.”

image
na MOSES SAGWEjournalist

Habari02 February 2025 - 10:44

Muhtasari


  • “Inashangaza sana jinsi Tanzania iliweka jina langu kwa watu wanaotafutwa Zaidi na Interpol. Rais Samia ana deni langu la msamaha,” Babu Owino aliandika.
  • Babu Owino pia alikariri kuwa bado amepigwa marufuku kutoka Uganda na haruhusiwi kukanyaga nchini humo.

MBUNGE wa Embakasi Mashariki amefichua kwamba safari yake ya hivi majuzi katika taifa la Tanzania iliishia kwake kuzuiliwa kwa Zaidi ya saa tatu akituhumiwa kuwa ni mmoja wa watu wanaotafutwa na Interpol.


Owino alifichua haya hivi majuzi wakati wa kikao chake cha mwanablogu Kogi kwenye chaneli yake.


Mbunge huyo alidai kwamba baada ya kutua katika uwanja wa ndege jijini Dar es Salaam, alishtukia akizuiliwa na kuonyeshwa kwamba jina lake lilikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakitafutwa na Interpol - shirika la kimataifa linalosaidia polisi kufanya kazi pamoja ili kupambana na uhalifu.


“Nilikwenda Tanzania, unajua nini kilitokea nilipofika Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam? Nilipowasilisha hati yangu ya kusafiria kwa ajili ya kibali cha uhamiaji waliandika, “Interpol Wanted List.” Sikuruhusiwa kuingia Tanzania, niliwekwa kizuizini huko kwa saa tatu kwa sababu walidai nilikuwa kwenye Orodha ya Wanaotafutwa ya Interpol ya Tanzania, nikasema sijawahi iba hata kuku, shida hap ani gani?” Babu alifunguka.


Alifuatisha klipu fupi kutoka kwa maongezi hayo kwenye kurasa zake mitandaoni akitoa wito kwa rais wa taifa hilo, Samia Suluhu Hassan kumuomba msamaha mara moja kwa kudhalilishwa kwake.


“Inashangaza sana jinsi Tanzania iliweka jina langu kwa watu wanaotafutwa Zaidi na Interpol. Rais Samia ana deni langu la msamaha,” Babu Owino aliandika.


Babu Owino pia alikariri kuwa bado amepigwa marufuku kutoka Uganda na haruhusiwi kukanyaga nchini humo.


"Nkienda Uganda nimepigwa marufuku, siwezi kukanyaga Uganda," alisema.


Serikali ya Uganda ilimpiga marufuku rasmi mbunge huyo wa Kenya kuingia nchini humo Mei 2019, na kumtangaza kuwa mtu asiyestahili.


Uamuzi huo ulitokana na kuhusika kwa Babu Owino kumkaribisha Bobi Wine wakati wa ziara yake nchini Kenya, ambapo wawili hao wanatuhumiwa kutoa matamshi ya uchochezi dhidi ya utawala wa Museveni.


Mbunge huyo mkosoaji mkali wa serikali ya rais Ruto alieleza kuwa hakufuatilia sana ya yaliyomkumba Tanzania, akisisitiza hana sababu ya kutembelea Tanzania.


"Nikienda Uganda nimepigwa marufuku, siwezi kuingia Uganda. Lakini kusema kweli, je, nahitaji chochote Tanzania? Ninahitaji nini Tanzania ambacho sipati Kenya? Sijasafiri hata hela nzima ya Tanzania? Kenya bado ninahitaji nini nchini Tanzania?" Babu alisema.


 



RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved