TAJIRI nambari moja duniani, Elon Musk amekuwa mtu maarufu kutoka nje ya Afrika wa kwanza kutia neno kauli ya rais mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta kuzitaka nchi za Afrika kuacha manung’uniko baada ya Marekani kutangaza mipango ya kusitisha misaada.
Kupitia ukurasa wa X, jukwaa
analolimiliki, Musk alinukuu video ya Kenyatta akirai mataifa ya Afrika kuacha
kulia baada ya Trump kutangaza misaada nje ya Marekani kusitishwa.
Kwa mujibu wa Musk, kauli ya Uhuru
Kenyatta ni nzuri si tu kwake bali pia kwa mataifa mengi ya Afrika ambayo
yamekuwa yakitegemea misaada ya mashirika na serikali ya Marekani kama USAID.
“Ni vizuri kwake,” Elon Musk alinukuu
video hiyo.
Mwishoni mwa mwezi uliopita wa
Januari, Uhuru Kenyatta akizungumza baada ya rais Trump kutangaza kusitishwa
kwa misaada ya kimatibabu kuja barani Afrika, aliwataka Waafrika kuacha
kulalamika kwa sababu Trump si rais wao.
Kwa mujibu wa Kenyatta, Waafrika
hawafai kunung’unika Amerika kukata misaada kwao kwani hawalipi kodi nchini
Marekani na wala Trump si rais wao.
"Niliona watu wengine siku
nyingine wakilia kwamba Trump ameondoa ufadhili. Si serikali yako, wala nchi
yako—mbona unalia?” Uhuru alipiga kwenye mshono.
“Hana sababu ya kukupa chochote;
haulipi ushuru huko Amerika. Huu ni wito wa kukuamsha kujua mtakachofanya ili
kujikimu,” Kenyatta alisema.
Kenyatta zaidi alisihi mataifa ya Kiafrika
kuanzisha mifumo ya kifedha inayojitegemea kushughulikia majanga kama vile
magonjwa ya milipuko, badala ya kuegemea wafadhili wa Magharibi.
Alisisitiza jinsi utegemezi wa kupita kiasi
wa usaidizi wa kigeni umedumaza maendeleo ya kiuchumi ya Afrika na utulivu wa
muda mrefu.
"Tutake au tusipende, ufadhili
wa haya (magonjwa) lazima utoke kwetu kwa sababu inabidi tuanze kutanguliza
tena kile ambacho ni muhimu kwetu kama Waafrika," Kenyatta alisisitiza.
Hata hivyo,
siku moja baada ya Trump kutangaza kusitishwa kwa misaada, alibatilisha amri
hiyo na kuruhusu misaada hiyo haswa ya kimatibabu kusambazwa kwa hadi mataifa
55 kote duniani yenye uhitaji mkubwa.