
MILKA Moraa Tegisi, mwanamke aliyevutia huruma nyingi mitandaoni wiki mbili zilizopita kufuatia video iliyoonyesha akidhalilishwa kanisani sasa ana kila sababu ya kutabasamu baada ya nyota ya jaha kumuangazia.
Moraa baada ya kudhalilishwa na kufukuzwa katika kanisa ya Neno Evangelism kwa kuomba msaada wa kodi ya nyumba, hali yake iliwagusa wengi ambao waliungana na kumchangia zaidi ya laki 3.
Kama hiyo haitoshi, Moraa sasa anatarajiwa kumiliki nyumba yake katika mtaa wa Mukuru katika miezi miwili ijayo, shukrani kwa Boma Yangu – mpango wa kumilikisha Wakenya nyumba za bei nafuu zinazojengwa na serikali.
Taarifa hii ilifichuliwa na waziri wa ardhi Alice Wahome ambaye alikutana na Moraa katika ofisi yake Jumatano.
Alisema kwamba aibu yake imegeuka na kuwa hadithi ya ufanisi wake na kwamba amesha andikishwa kwenye mpango wa Boma Yangu tayari kukabidhiwa nyumba baada ya malipo kukamilika.
Waziri Wahome alisema kwamba Moraa atakuwa mmiliki mpya wa nyumba ya kifahari ya mradi wa serikali wa nyumba za bei nafuu ambayo itakuwa na jikoni, bafu na choo cha ndani.
“Milka Moraa alianza kuvuma mtandaoni baada ya tukio la bahati mbaya la udhalilishaji hadharani kusambaa. Asubuhi ya leo pale Ardhi House, nilikutana na Milka Moraa ambaye alinieleza safari yake ya kufika alipo sasa, pia tulijadili usajili wake kwenye Mpango wa Nyumba za bei nafuu kupitia Boma Yangu, ambapo amelipa amana yake na ataendelea kulipa kadri anavyopanga ili kumiliki.”
“Katika muda wa miezi miwili, Milka sasa anatazamiwa kumiliki nyumba ya kujitegemea katika Mukuru Site, ambayo imekamilika na huduma muhimu, ikiwa ni pamoja na jiko, bafu na choo,” waziri Wahome alisema.
Waziri huyo pia alimshukuru afisa wa polisi Sammy Ondimu Ngare ambaye aliongoza wanamitandao katika kuchangisha zaidi ya laki 3 kumsaidia Moraa.
Kando na michango, Ngare alihakikisha mama huyo amepata kazi katika mgahawa mmoja jijini Nairobi.
“Shukrani za dhati kwa Sammy Ondimu Ngare kwa kudhihirisha hadithi yake na kumuunga mkono kupitia mchakato wa uwekaji kumbukumbu.”
Wahome pia alikariri matamshi ya mchungaji Ng’ang’a ambaye wakati anamfukuza Moraa kanisani alimtaka kuenda kupata nyumba kwa serikali.
“Lazima pia nimtambue Mchungaji Ng’ang’a kwa kumwelekeza Milka kwenye Nyumba ya bei nafuu, asante sana,” alimaliza.