
KIONGOZI wa chama cha ODM ambaye pia ni mgombea wa wadhifa wa uenyekiti wa bara la Africa, AUC, Raila Odinga ameonyesha utayarifu wake kuelekea uchaguzi huo zikiwa zimesalia siku 4 pekee.
Akizungumza katika mkutano mkuu wa ODM ulioandaliwa katika
ukumbi wa Bomas jijini Nairobi leo Jumatatu, Odinga alisema kwamba kujitokeza
kwake kuwania kulitokana na msukumo kutoka kwa viongozi wa Afrika.
Odinga alisema kwamba alishawishiwa na baadhi ya viongozi wa
Afrika kuwania wadhifa wa uenyekiti wa AUC kwani walimuona kama suluhisho bora
kwa matatizo ya bara hili.
“Viongozi wa Afrika
waliniambia wananitaka katika Afrika, Afrika iko na shida nyingi zaidi. Wakasema
shida ambayo mko nayo Kenya ndio iko Nigeria, Ghana na kwingineko. Kwa hivyo
ukija hapa juu tupate suluhisho tutaliweka katika nchi zote za Afrika.”
“Wakaniuliza, ‘kubali uje
uwe kama kiongozi wa bara la Afrika’. Nikapiga moyo konde nikajiuliza na Kenya
je? Nikasema Kenya iko ndani ya Afrika nan iko tayari kujaribu.”
Odinga alisema ni kutokana na msukumo huo ndio maana ametoka
na kukutana na viongozi wote na kusema kwamba kama watakubali basi atakuwa
mwenyekiti wa AUC.
Kiongozi huyo wa muda mrefu katika siasa za Kenya pia alisema
kwamba hana wasiwasi wowote katika matokeo ya aina yoyote, akiradidi kwamba
yuko tayari kwa lolote.
“Kwa hiyo mimi nimetoka
nimeongea na viongozi wote wa bara la Afrika, wakikubali nitakuwa mwenyekiti wa
AU.”
“Kura itapigwa Jumamosi
hii inayokuja, mimi naenda, nikichaguliwa sawa na nisipochaguliwa sawa. Sivyo? Si
mimi niko na nyumbani kwetu?” Odinga alisema.
Alimalizia kwa kuwashukuru Wakenya kwa kumuombea na kumtakia
mema katika matokeo ya uchaguzi huo utakaofanyika wikendi.
“Ahsanteni sana kwa
kuniombea, mimi nitasimama imara na nikienda katika bara la Afrika, nitafanya
mambo laini kisawasawa vile nyinyi mnajua tabia yangu,” alisema.
Raila atachuana na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Djibouti
Mahamoud Ali Youssouf na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Madagascar Richard
Randriamandrato.
Wadadisi wanasema tishio kubwa la Raila ni mgombeaji wa
Djibouti, ambaye anaaminika kuungwa mkono na nchi za Kiislamu na Kiarabu.