
WAKAAZI wa kijiji cha Kilimani kaunti ya Kakamega waligubikwa na butwaa kufuatia mkasa wa mauaji ya kifamilia.
Kwa mujibu wa ripoti, vijana wawili ambao ni kaka wa
toka-nitoke walizozania kiasi cha ugali ambacho wangepika kupelekea mmoja wao
kuuawa na mwenzake.
Reuebn Lutaboni mwenye umri wa miaka 42 alizozana na kakake
mdogo Michael Lukala mwenye miaka 40 kuhusu kiasi cha ugali ambacho
wangestahili kupika wakati Lutaboni alimshambulia mwenzake na kumuua.
“Wawili hawa walikuwa ni
marafiki ambao wangefanya vibarua kijijini na walirudi nyumbani kupika chajio
wakati mzozo ulipotokea. Mmoja alikuwa anapika wakati mwenzake alimshambulia na
shoka kichwani mara kadhaa. Alimgonga kwa ubongo karibu mara 5, upande wa macho
akamgonga mara 3 halafu upande wa macho akakata kabisa na kummaliza,” ndugu mkubwa alisema.
Cleophas Barasa, mzee katika kijiji hicho alilaani kitendo
hicho huku akitoa wito kwa watu kutatua tofauti zao kwa njia zifaazo kuliko
vita.
“Mambo kama haya ya
chakula haistahili ndugu kupigana mpaka mwingine anaua mwenzake kwa sababu ya
chakula. Watu ambao wako zaidi ya umri wa 40 kuishi pamoja pia ni hatari kwa
sababu hujui ni nini kitatokea baadae,” mzee huyo alishauri.