
WINNIE Byanyima, mke wa mwanasiasa wa muda mrefu katika siasa za upinzani nchini Uganda Kizza Besigye ametangaza kuwa anaandika kitabu, na sehemu yake itaangazia uhusiano wake wa zamani na Rais Yoweri Museveni.
Byanyima ambaye ni mkurugenzi katika shirika la misaada la
Marekani la kupambana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI, UNAIDS alisema haya
kupitia ukurasa wake wa X alipokuwa akijibu baadhi ya watu wanaojadili kwa njia
hasi kuzuiliwa kwa mume wake.
Mwanamke huyo alikuwa akijibu mjadala kwenye NBS TV, ambapo
mwanahabari mkongwe Andrew Mwenda aliachana na mada ya madai ya Kizza Besigye
kuzuiliwa kinyume cha sheria ili kuanzisha uhusiano wake na Museveni.
Byanyima alimjibu akisema kwamba ikiwa anavutiwa na simulizi
ya uhusiano wake wa zamani na Museveni, basi anafaa kusubiri hadi pale yeye
[Byanyima] atakapoachilia kitabu chake ili kupata uhondo zaidi.
"Ikiwa ni ya kupendeza kwake, anapaswa kungojea kitabu changu, ni hadithi ya kupendeza!" Byanyima alichapisha kwenye X.
Byanyima anaaminika kuwa alikuwa na historia ya kimapenzi na
Museveni kabla ya kuolewa na Kizza Besigye mnamo Julai 7, 1999, huko Nsambya,
Kampala.
Wanandoa hao wana mtoto wa kiume, Anselm Besigye, ambaye kwa
sasa anafuata PhD katika Chuo Kikuu cha Columbia huko New York.
Baadae Ijumaa, Besigye alipata nafuu baada ya kesi yake
kuhamishwa kutoka mahakama ya kijeshi hadi katika mahakama ya kiraia ambapo
alifunguliwa shtaka la uhaini ambalo adhabu yake ni kifo.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, Besigye
amekuwa akisusia chakula kwa takribani wiki 2, ishara ya kupinga kufunguliwa
mashtaka katika mahakama ya kijeshi sasa amerejelea chakula.
Besigye, mgombea urais mara nne katika nchi hiyo ya Afrika
mashariki, alikaa kwenye kiti cha magurudumu alipokuwa akikabiliwa na mashtaka
katika chumba cha mahakama katika mji mkuu, Kampala.
Besigye, 68, amekuwa kizuizini tangu Novemba 16,
alipotoweka katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.
Siku kadhaa baadaye, alifikishwa mbele ya mahakama ya
kijeshi mjini Kampala kujibu mashtaka ya kutishia usalama wa taifa.
Mahakama ya Juu ilisimamisha kesi yake ya kijeshi mwezi
uliopita, ikisema jopo la mahakama ya kijeshi haliwezi kuwahukumu raia.
Familia ya Besigye, wafuasi na wengine walitaka aachiliwe
mara moja, lakini aliwekwa katika gereza lenye ulinzi mkali na baadaye kuanza
mgomo wa kula.