
MWAKILISHI wadi wa Kileleshwa, Robert Alai amewataka vigogo wa chama cha ODM, gavana wa Siaya James Orengo na mwenzake wa Kisumu Anyang’ Nyong’o kujiondoa katika siasa za eneo la Luo Nyanza akidai kwamba hakuna lolote la maana wamewahi fanya.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Alai
alisema kwamba Orengo mwenye umri wa miaka 74 na Nyong’o mwenye miaka 79 ni
wanarika na kiongozi wa ODM Raila Odinga lakini athari yao kimaendeleo ni finyu
mno ikilinganishwa na Odinga mwenyewe.
Alisema kwamba ni wakati umefika wawili hao
‘kufa na kuzikwa’ kisiasa ili kutoa nafasi kwa viongozi wachanga wenye maoni
kuhudumia watu wa Luo Nyanza na kuwaokoa kutoka taabu na umaskini.
“Nyongo na Orengo wana umri wa miaka
79 na 74 mtawalia. Ni wanarika wa Raila Amolo Odinga. Hawatakuonyesha jambo
lolote la maana walilofanya kuwainua vijana wa Kijaluo kutoka katika taabu na
umaskini. James Orengo na Anyang Nyong'o lazima wafe kisiasa mara moja na
wazikwe. Sioni thamani katika siasa zao!,” Alai
alisema.
MCA huyo aliendelea kuwalaumu wawili hao
kwa kile alidai kwamba kazi yao imekuwa ni kuwatumia vijana Wajaluo kwa
maandamano kwa faida zao wenyewe, akisema kuwa bila Raila Odinga, wote hawako.
“Wameishi maisha ambayo wanajua tu
kupeleka vijana wa Kijaluo kufia mitaani ili hata mabilioni yao yaongezeke.
Orengo na Nyong'o wananing'inia kwenye koti la Raila wakiwa na wazo gumu sana
la nini Wajaluo wanapaswa kufanya ili kufa kwa ajili ya Kenya na kuleta
mabadiliko ya kimawazo ambayo wao wenyewe wameyapata.”
“Leo ukiuliza Orengo au Nyong'o ni nani mbadala wao kutoka kwa Ruto, hawatafikiria zaidi ya Baba Raila Odinga. Hawana wazo! Hawana fununu ya kile ambacho watu wanapaswa kufanya ili kufikia nirvana wanayofikiria,” Alai aliongeza.
Aidha, malalamishi yake hayakumsaza katibu
mkuu wa ODM Edwin Sifuna ambaye baadhi ya wanachama wanahisi anatumika kisiasa
na aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua.
Tetesi za Sifuna kuvutia upande wa Gachagua
kisiasa ziliibuliwa na George Aladwa, mbunge wa Makadara ambaye pia ni
mwenyekiti wa chama hicho tawi la Nairobi.
Aladwa alimuonya Sifuna kwamba huenda hivi
karibuni akatimuliwa kama katibu wa ODM kama ambavyo mtangulizi wake Ababu
Namwamba alivyofanyiwa.