
Naibu Rais Kithure Kindiki amewataka wakazi wa Mlima Kenya kumpuuza mtangulizi wake aliyetimuliwa, Rigathi Gachagua.
Kindiki alimtaja Gachagua kama mkandamizaji ambaye alishindwa kutoa matokeo yanayoonekana akiwa afisini na ameanza kutumia maneno ya migawanyiko.
Akihutubia mkutano katika nyumba yake ya mashambani ya Irunduni katika Kaunti ya Tharaka Nithi, Kindiki alimkemea mtangulizi wake aliyetimuliwa, na kumtahadharisha dhidi ya kumuingiza kwenye vita visivyo vya lazima vya kisiasa.
Alipuuzilia mbali makabiliano hayo na kusema kuwa ni kero tu, akisema hana muda nayo kwa vile anabakia kulenga kulitumikia taifa.
"Naona watu wengine wanataka tujibizane... I’m busy... waambieni hiyo tabia mbaya wakome... hii madharau mingi wajue we are not pushovers... amekutana na watu watano sijui ishirini na wanajigamba... sisi tunaweza kuita maelfu ya watu," alisema Kindiki.
Kindiki alikuwa akizungumza baada ya kuwakaribisha viongozi wa mashinani kutoka Kaunti za Embu, Meru, na Tharaka Nithi, ambapo alipuuza dhihaka za Gachagua kuwa yeye ni mtu wa ndiyo, akiwataka Wakenya kupuuza viongozi kama hao.
Aliwataka wakaazi wa eneo la Mlima Kenya kukataa majaribio ya Gachagua ya kuwachochea dhidi ya serikali, akionya kuwa vitendo kama hivyo vinaweza kutenga eneo hilo kutoka kwa miradi ya maendeleo inayoendelea.
"Msikubali hila za wanasiasa wenye nia mbaya... leo, hata kama singekuwa DP, ningeunga mkono maendeleo ya eneo hili," aliongeza.
Aidha amewahakikishia wananchi kuwa serikali imepata rasilimali za kukamilisha miradi yote iliyokwama, ikiwemo barabara, masoko na usambazaji wa umeme vijijini, akisisitiza dhamira ya uongozi katika kuboresha maisha.
"Nina habari njema kwa watu wetu na habari mbaya kwa wapinzani... serikali imefanikiwa kupata fedha za kumaliza miradi yote... kazi sasa imeanza," Kindiki alisema.
Kindiki alitoa wito kwa Wakenya kusalia makini na kuungana nyuma ya ajenda ya maendeleo ya serikali, akithibitisha kuwa maendeleo yanayoonekana yanaendelea. Pia alidokeza sherehe ya kurudi nyumbani katika wiki zijazo.