
Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi amesema hataandamana na Rais William Ruto katika ziara yake iliyopangwa katika eneo la Mlima Kenya.
Muturi alisisitiza kuwa si kawaida yake kumfuata rais kwenye ziara, akibainisha kuwa hata wakati wa utawala wa aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta, hakuwa na mazoea ya kuandamana naye.
“Simfuati rais tu... Hata wakati Uhuru akiwa rais na mimi nikiwa spika, haikuwa kawaida yangu wala mazoea kumfuata kila alikokwenda,” alisema.
Akizungumza baada ya mkutano na wazee wa Kikuyu huko Kiambu Jumamosi, Muturi alifafanua kuwa ataandamana tu na Ruto ikiwa ziara hiyo itahusiana moja kwa moja na majukumu yake ya uwaziri.
Waziri huyo amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali, hata kuruka mikutano ya Baraza la Mawaziri.
Katika mahojiano ya hivi majuzi, alifichua kuwa alimwomba rasmi Rais Ruto amsamehe kuhudhuria vikao vya Baraza la Mawaziri hadi suala la utekaji nyara na mauaji ya kiholela lipewe kipaumbele kwa majadiliano.
"Kuhudhuria mikutano ya Baraza la Mawaziri ni lazima isipokuwa mtu awe na kibali kutoka kwa Rais, jambo ambalo nilitaka," Muturi alisema.
Alisisitiza kuwa uamuzi wake haukuwa wa ukaidi, kwani alimwandikia barua mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri akiomba msamaha.
Muturi hajahudhuria vikao vyovyote vya Baraza la Mawaziri tangu alipoikosoa serikali hadharani kuhusu utekaji nyara, suala ambalo lilijiri nyumbani wakati mwanawe, Lesly Muturi, alipotekwa nyara akiwa na marafiki zake, akiwemo Mbunge wa Embakasi Magharibi Mark Mwenje.
Kufuatia kutekwa nyara kwa mwanawe, Muturi alisema alikutana na Rais Ruto, ambaye aliwasiliana na Mkurugenzi wa Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS) Noordin Haji, na kusababisha Lesly kuachiliwa.