
KIONGOZI wa chama cha People’s Liberation Party, PLP Martha Karua amedokeza kwamba ni wakati sasa Kenya kuongozwa na rais mwanamke.
Akizungumza Jumatatu katika kaunti ya Isiolo, Karua aliweka
wazi nia yake ya kuwania urais, akisema kwamba atalitunza taifa la Kenya kwa
njia sahihi ya upendo kama jinsi ambavyo mama hutunza boma lake.
“Kile kiti mimi nataka ni
cha urais. Na ndivyo kama mama niweze kutunza Kenya vile ambavyo mama hutunza
boma. Mama hawezi kuacha mtoto hata mmoja kulala njaa. Hata chakula kikiwa
kidogo mama anagawa kidog-kidogo ili kila mmoja apate, hata mtu wa kupita anapatiwa yake
kidogo,” Martha Karua alisema.
Kiongozi huyo ambaye tangu kusambaratika kwa uliokuwa
muungano wa upinzani wa Azimio amekuwa akiikosoa serikali mara kwa mara amekuwa
akionekana kuweka hai matumaini yake ya kuliongoza taifa.
Alisema kwamba Kenya ina utajiri wa kipekee ambao unafaa
kumfaidi kila mwananchi, akionekana kuashiria kwamba ilivyo kwa sasa, kuna
upendeleo katika ugavi wa raslimali za taifa.
“Keki ya Kenya tunataka
igawe kwa usawa, sio vile ilivyo siku hizi. Mmejaribu wanaume huo wakati wote
lakini safari hii nawaomba mjaribu mama kupitia PLP,” Karua alirai wananchi.
Karua ameonekana kukubali Ushirikiano na viongozi wengine wa
upinzani akiwemo aliyekuwa naibu wa rais Rigathi Gachagua na Kalonzo Musyoka
katika kuzindua muungano dhabiti wa kushindana na rais Ruto katika uchaguzi wa
urais 2027.
Cha ajabu ni kwamba licha ya viongozi hao wote kuonekana kuwa
na nia ya kufanya kazi pamoja, kila mmoja wake kwa wakati wake amekuwa akiweka
wazi kwamba atawania urais 2027.