
Mahakama Kuu imeagiza Mamlaka ya Mawasiliano (CA) kurejesha mawimbi yote ya matangazo ya vituo vya televisheni vya NTV na KTN.
Jaji Chacha Mwita alisema kwamba kushindwa kutekeleza agizo hilo kutapelekea wasimamizi wa CA kufunguliwa mashtaka.
Mapema hii leo, serikali iliamuru vyombo vyote vya habari vinavyoendesha vituo vya televisheni na redio nchini Kenya kusitisha kuonyesha mubashara maandamano yanayoendelea nchini humo, huku Chama cha Wahariri nchini humo (KEG) kikikosoa uamuzi huo.
Katika agizo lililotolewa tarehe 25 Juni, Mkurugenzi Mkuu wa CA, David Mugonyi, alitaja ukiukaji wa Kifungu cha 33(2) na 34(1) cha Katiba ya Kenya, pamoja na Sehemu ya 461 ya Sheria ya Mawasiliano na Habari ya Kenya ya mwaka 1998, kuwa msingi wa marufuku hiyo.
“Matangazo ya moja kwa moja ya maandamano ya Juni 25, 2025 ni kinyume na Kifungu cha 33(2) na 34(1) cha Katiba ya Kenya na Sehemu ya 461 ya Sheria ya Mawasiliano na Habari ya Kenya,” ilisomeka taarifa hiyo.
Mamlaka hiyo ilionya kuwa kutotii agizo hilo kutasababisha kuchukuliwa hatua za kisheria kulingana na sheria.
“Vituo vyote vya runinga na redio vinaelekezwa kusitisha mara moja matangazo yoyote ya moja kwa moja ya maandamano. Kutozingatia agizo hili kutasababisha hatua za kisheria kama ilivyoelekezwa,” ikaongeza.
Nation Media Group ilitoa taarifa awali ikisema kuwa kituo chao cha runinga cha NTV kimezimwa na Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya (CA).
"Polisi na Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya waliingia kwa nguvu katika kituo cha matangazo cha NTV kilichoko Limuru na kuzima ishara ya matangazo ya bure (Free-to-Air)," ilisomeka taarifa ya shirika hilo la habari.
Tukio hilo lilijiri dakika chache baada ya CA kutoa agizo kwa vituo vyote vya runinga na redio kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya maandamano ya kizazi cha Gen Z yanayoendelea kote nchini.
Chama cha Wahariri Kenya (Kenya Editors Guild) kimekemea agizo hilo la CA la kupiga marufuku matangazo ya moja kwa moja ya maandamano, likilitaja kama ukiukaji mkubwa wa Katiba na uhuru wa vyombo vya habari.
Kwa upande mwingine, Standard Media Group ilitoa taarifa ikisema kuwa hawajapokea barua yoyote kutoka kwa Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya inayowaagiza kusitisha matangazo ya maandamano yanayoendelea.
Hii si mara ya kwanza kwa CA kutishia kuviondoa vituo vya runinga hewani. Vitisho kama hivyo vilitolewa mwaka jana, wakati wa kilele cha maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha wa 2024 ambapo waandamanaji walivamia Bunge.”