
Waziri wa zamani wa Usalama wa Ndani, Dkt. Fred Matiang’i, amelaani hatua ya polisi kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji.
Matiang’i alitoa matamshi hayo kufuatia ripoti kwamba angalau watu saba waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa wakati wa maandamano ya Jumatano yaliyofanyika kuwaenzi waandamanaji wa kizazi cha Gen Z waliouawa kwa kupigwa risasi na polisi mwaka uliopita.
Waandamanaji hao walikuwa miongoni mwa wale waliokuwa wakieleza wasiwasi wao kuhusu Mswada wa Fedha wa 2024, sera kandamizi za ushuru, usimamizi mbaya wa rasilimali za umma, kupunguzwa kwa ufadhili wa serikali kwa vyuo vikuu, na masuala mapana ya utawala.
“Katika kufanya hivyo, hawa raia vijana waliokuwa na ari walikuwa wakitumia haki yao ya kikatiba ya kuwasilisha malalamiko yao kwa mamlaka. Ninaunga mkono kikamilifu hisia walizotoa. Naishauri serikali isifumbe moyo wake bali isikilize kwa dhati kilio cha wananchi kuhusu haki na mageuzi,” alisema Matiang’i.
“Matumizi ya nguvu na mamlaka yatazidisha tu mgogoro na kuiweka nchi kwenye mwelekeo wa hatari na wa utelezi. Pole zangu za dhati ziende kwa familia zilizopoteza wapendwa wao katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita chini ya hali hizi za kusikitisha,” alisema Matiang’i.
Aliwataka Wakenya wa mitazamo yote ya kisiasa kuweka kando tofauti zao na kushikamana kupigania ukombozi wa nchi dhidi ya uongozi wa kifisadi.
“Lazima tuungane kuvuka mipaka ya vyama vya siasa na vizazi, kurekebisha yaliyoharibika na kujenga mustakabali wa haki, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wote.”
Aliwahimiza polisi kuwa na kiasi wanapokabiliana na waandamanaji.
“Pia ninatoa ombi la dhati kwa maafisa wetu wa usalama: tafadhali msielekeze silaha zenu kwa wananchi wenzenu. Kuweni na kiasi na busara. Msikabiliane na maandamano ya amani kwa kutumia nguvu.”
“Ni kupitia tu mazungumzo na utayari wa kweli wa kusikiliza ndipo tutakapoweza kupata njia ya kusuluhisha malalamiko kwa amani na kurejesha utulivu katika taifa letu tunalolipenda.”