
Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, ametangaza kuwa serikali haijatenga bajeti yoyote ya kuwafidia waathiriwa ambao mali zao ziliibwa au kuharibiwa wakati wa maandamano ya Jumatano, Juni 25.
Akizungumza na wanahabari, Murkomen alieleza kuwa Bunge linapaswa kutunga sheria itakayofafanua fidia kwa waathiriwa wa aina hiyo na kuweka adhabu kali zaidi kwa waandalizi wa maandamano.
Alisisitiza haja ya kudhibiti maandamano ili kuwaweka waandalizi kwenye wajibu iwapo mali itaharibiwa au kuibwa.
"Kwa bahati mbaya, Bunge halijatenga bajeti ya kuwafidia wale ambao mali zao ziliibwa katika hali kama hizi, na sisi kama serikali hatuna mgao wowote wa kufanya hivyo," alisema.
"Ikiwa tungekuwa na bajeti ya kuwafidia watu kila mara mali zao Zimbabwe, basi sheria bora zaidi ni kwamba waandalizi wa maandamano wachukue jukumu kuu."
"Ndiyo maana tunasisitiza kuwepo kwa sheria inayofafanua waandalizi watafanyia maandamano yao wapi, saa ngapi na mahali gani. Mombasa ni mfano wa jinsi maandamano ya umma yanavyopaswa kufanyika."
Hata hivyo, alieleza kuwa viongozi binafsi watachangia kwa njia ya msaada kwa wale waliopoteza mali nyingi.
Aidha, Waziri huyo alidai kuwa 'wahuni' walizua machafuko hadi usiku wa manane na kuwanyang’anya raia waliokuwa wakielekea nyumbani.
"Uharibifu uliendelea hadi usiku wa manane. Wahuni waliletwa kutoka Murang’a, Nyeri, Kirinyaga na wakaachwa mjini, wengine Barabara ya Thika, na walipokuwa wakirudi nyumbani, wakaanza kusababisha fujo na machafuko. Polisi walizidiwa," alibainisha.
"Haijakuwa rahisi wakati kundi kubwa la wahuni, wahalifu, majambazi na waporaji wanapokusanywa mahali pamoja na wanasiasa."
Kwa mujibu wa Murkomen, mali ya thamani ya mabilioni iliharibiwa wakati wa maandamano ya jana, akisema kuwa wahuni walilenga maduka makubwa ya rejareja, maduka ya vifaa vya kielektroniki na mikahawa.