
Rais William Ruto, siku ya Alhamisi tarehe 26 Juni 2025, alitia saini Mswada wa Fedha wa mwaka 2025 kuwa sheria katika Ikulu ya Nairobi.
Mswada huo, uliopitishwa na Bunge la Kitaifa mnamo Juni 19, 2025, ulipendekeza mabadiliko mbalimbali katika Sheria ya Kodi ya Mapato, Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), Sheria ya Taratibu za Kodi, Sheria ya Ada na Tozo Mbalimbali, Sheria ya Ada ya Stempu, na Sheria ya Ushuru wa Bidhaa.
Pendekezo moja muhimu katika Sheria ya Kodi ya Mapato ni kuanzishwa kwa kikomo cha miaka mitano kwa kuhamisha hasara ya kodi kwenda miaka ijayo. Hapo awali, walipa kodi waliruhusiwa kuhamisha hasara hizo bila kikomo, hatua iliyotoa nafasi ya kujikinga na faida za baadaye kwa muda mrefu.
Chini ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, mabadiliko ya kipekee ni hitaji la kuwa na ankara ya kodi kwa kila aina ya usambazaji, ikiwemo zile bidhaa na huduma zisizotozwa kodi. Hii inapanuwa wigo wa masharti ya utoaji wa ankara na kuhitaji biashara kuwa na mfumo uliosanifiwa kwa bidhaa na huduma zote, zenye kodi na zisizo na kodi.
Aidha, Mswada huo unawataka waajiri kutumia moja kwa moja nafuu, makato, na misamaha yote inayotakiwa wakati wa kuhesabu kodi ya mapato ya wafanyakazi (PAYE), kwa lengo la kuongeza usahihi na kuboresha mshahara halisi wa mfanyakazi kwa kuhakikisha manufaa hayo yanatumika mapema.
“Kipengele hiki kitahakikisha kwamba wafanyakazi wanapata manufaa yao yote ya kodi bila haja ya kutoa madai tofauti, jambo ambalo litaboresha uzingatiaji wa sheria na usawa katika mfumo wa kodi,” alisema Kuria Kimani, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Fedha na Mipango ya Kitaifa.
Mswada wa Fedha wa 2025 pia unaanzisha mabadiliko katika Sheria ya Ushuru wa Bidhaa na Sheria ya Ada na Tozo Mbalimbali.
Kati ya mabadiliko hayo ni kufutwa kwa Kodi ya Mali ya Kidijitali na badala yake kuwekwa ushuru wa bidhaa wa asilimia tano kwa ada za miamala zinazolipwa kwa watoa huduma za mali pepe, pamoja na ushuru wa bidhaa wa asilimia 10 kwa ada za huduma za mali pepe, kwa lengo la kuchochea uchumi wa kidijitali.
Vivyo hivyo, kuna marekebisho yanayohusu bidhaa na huduma maalum, ikiwemo ushuru wa bidhaa wa asilimia tano kwa amana zinazowekwa kwenye pochi za kamari, michezo ya kubahatisha, na bahati nasibu, hatua inayoonyesha juhudi za kupanua wigo wa kodi na kuongeza mapato kutoka kwa sekta mpya zinazokua kwa kasi.
Hafla ya kutiwa saini kwa sheria hiyo ilishuhudiwa na wafanyakazi wa Ikulu pamoja na wawakilishi kutoka Bunge.
Waliohudhuria walijumuisha Spika Moses Wetang’ula, Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah, Kiongozi wa Wachache Junet Mohamed, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Ugawaji wa Fedha katika Bunge la Kitaifa Samuel Atandi, na Mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo, miongoni mwa viongozi wengine.
Sheria ya Fedha ya 2025 inatarajiwa kupanua wigo wa kodi na kurahisisha mfumo wa ukusanyaji mapato, hasa ikizingatiwa kuwa mswada wa awali wa mwaka 2024 ulikataliwa baada ya kupitishwa kwa mabishano makali bungeni, jambo lililosababisha upinzani mkali kutoka kwa wananchi.