
Mshirika wa karibu wa Rais William Ruto, Farouk Kibet, ametoa wito kwa Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen na Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) kuchukua hatua dhidi ya wahalifu waliopora mali wakati wa maandamano.
“Ningependa kumwomba Waziri Murkomen na wakuu wa idara ya polisi kuwakamata na kuchukua hatua kali dhidi ya wahuni waliopora mali ya Wakenya wakati wa maandamano,” alisema Farouk Kibet.
Wakati huo huo, wanasiasa wanaoegemea kwa serikali ya muungano mpana wanatoa wito wa kukamatwa kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kutokana na madai ya kuhusika na machafuko yaliyojitokeza wakati wa hafla ya ukumbusho wa Gen Z iliyofanyika Jumatano, Juni 25.
Wakiongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, Kiongozi wa Wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot, na mshauri wa Rais Ruto, Farouk Kibet, viongozi hao walilaani vurugu hizo, wakizitaja kama "ugaidi uliopangwa" na upinzani.
"Mtu yeyote anaweza kuandamana, kupiga kambi au kuwasilisha ombi kwa ofisi yoyote. Sasa, kwa yale yaliyotokea Jumatano, nilitaka kusikia maaskofu wakieleza iwapo waliona machafuko yale na kama waliona kama ilikuwa sawa," alisema Wetang’ula.
Walimtaka Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) na Idara ya Mahakama kuchukua hatua za haraka, wakilaumu upinzani kwa uchochezi, uharibifu wa mali na upotevu wa maisha.
"Mwaka jana, kulikuwa na maandamano Liverpool. Ndani ya wiki tatu, wote waliovunja mali walipelekwa jela. Wiki mbili zilizopita, kulikuwa na maandamano Los Angeles, na tunavyoongea leo, wote waliovunja mali ya umma wako jela," alieleza Cheruiyot.
Haya yanajiri huku viongozi wa Kenya Kwanza wakimtuhumu Gachagua kwa kuchochea vurugu kwa kuwataka vijana waandamane mitaani.
Kwa upande wake, aliyekuwa Naibu Rais alimlaumu aliyekuwa bosi wake, Rais William Ruto, kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji wasio na silaha, akisema kuwa taifa limegeuzwa kuwa dola ya kipolisi.
"Kwa maneno makali kabisa, nalaani matumizi ya nguvu kupita kiasi na risasi za moto na Polisi dhidi ya waandamanaji wa Gen Z waliokuwa na amani na hawakuwa na silaha, kama ilivyoshuhudiwa jana kote nchini," alisema Gachagua katika taarifa yake ya Juni 26, 2025.