
Dennis Itumbi, mkuu wa Miradi Maalum ya Rais na Uchumi wa Ubunifu, amemsifu David Mugonyi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya (CA), kwa kuzima masafa ya vituo vya runinga vilivyokuwa vikipeperusha moja kwa moja maandamano ya Jumatano.
Akilitaja suala hilo kama tendo la “uzalendo chini ya shinikizo,” Itumbi alisisitiza kuwa Mugonyi hakudhibiti uhuru wa vyombo vya habari, bali alilinda uthabiti wa taifa.
“Mugonyi alichukua hatua sahihi. Haikuwa udhibiti wa habari. Uhuru wa vyombo vya habari unaweza kuwepo tu ikiwa tuna taifa. Kenya kwanza. Ilikuwa ni uzalendo chini ya shinikizo,” alisema Itumbi.
“Kama mwanahabari, haikuwa uamuzi mwepesi. Alijua vichwa vya habari vingesema nini. Alielewa uzito wa kamera, matarajio ya vyumba vya habari, na usambazaji mkubwa mtandaoni, lakini Kenya ilimuhitaji,” aliongeza.
Itumbi alisifu hatua hiyo ya Mugonyi kama “uamuzi wa kishujaa na wa kizalendo” uliolenga maslahi ya taifa, kupitia taarifa aliyoichapisha mtandaoni.
“Waandamanaji walikuwa tayari wamechoma vituo vya polisi, kupora na kuharibu mali, uwekezaji, ndoto na matarajio katika maeneo ya Nairobi, Nyeri na Embu, na maeneo yaliyo chini ya ulinzi yalikuwa hatarini. Vyombo vya habari kama ilivyotarajiwa vilielekeza kamera moja kwa moja, vikiongeza moto badala ya kuutuliza. Kwa wakati huo, Mugonyi, kwa mtazamo wangu, alichagua nchi badala ya machafuko.
“Alimchagua Kenya, kwa sababu bila taifa, hakuna chumba cha habari cha kujadili kutoka, hakuna studio ya kurusha matangazo, hakuna uhuru wa vyombo vya habari wa kutetea.”
Akitambua upinzani alioupata, Itumbi alimhimiza Mugonyi asikate tamaa ikiwa hali kama hiyo itajirudia.
“Tafadhali, ndugu Mugonyi, kama wakati kama huo utatokea tena, usisite kuichagua Kenya tena. Kila wakati. Daima,” aliandika.
Aidha, Itumbi aliikosoa baadhi ya redio na runinga kwa madai ya kuchochea taharuki badala ya kuelimisha umma.
“Kwa hali ilivyo, baadhi ya vyumba vya habari vinaonekana kana kwamba ni vyama vya kisiasa visivyosajiliwa, si waandishi wa habari. Mugonyi, umefanya vyema. Iwapo hali kama hiyo itatokea tena, tafadhali chagua Kenya. Kila wakati. Daima,” alisema.
Licha ya mjadala mkali wa umma, Itumbi alisisitiza kuwa hatua ya Mugonyi inafanana na maamuzi yaliyowahi kuchukuliwa na serikali nyingine duniani zilizokumbwa na machafuko kama hayo, na hivyo inapaswa kutazamwa kwa jicho la kizalendo.
“Kote duniani, maamuzi kama hayo yamewahi kufanywa:
“Baada ya tukio la 9/11, mitandao ya runinga ya Marekani ilisitisha kila kitu, na kuungana na maslahi ya taifa kabla ya kuangalia viwango vya watazamaji,” alieleza.
“Wakati wa mashambulizi ya London ya tarehe 7/7, vyombo vya habari vya Uingereza vilishirikiana na mamlaka kuzuia hofu zaidi. Mnamo 2008 huko Mumbai, India ilijifunza kwa uchungu kwamba matangazo ya moja kwa moja yanaweza kuhatarisha maisha. Christchurch 2019, vyombo vya habari vya New Zealand vilizuia kurusha picha za moja kwa moja ili kuepuka kueneza propaganda za misimamo mikali,” aliongeza.
“Wakati wa janga la Norway la mwaka 2011, watangazaji wa Norway walizingatia kuunganisha taifa badala ya kumpa umaarufu mshambuliaji. Rwanda 1994, dunia ilishuhudia gharama kubwa ya uchochezi wa vyombo vya habari.”
Katika agizo lililotolewa Juni 25, Mugonyi alitaja ukiukaji wa Kifungu cha 33(2) na 34(1) cha Katiba, pamoja na Kifungu cha 461 cha Sheria ya Mawasiliano na Habari ya Kenya ya mwaka 1998, kama msingi wa marufuku hiyo.
“Matangazo ya moja kwa moja ya maandamano ya tarehe 25 Juni 2025 ni kinyume na Kifungu cha 33(2) na 34(1) cha Katiba ya Kenya na Kifungu cha 461 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kenya,” ilisomeka taarifa hiyo.
CA baadaye iliondoa marufuku hiyo kufuatia agizo la mahakama lililosimamisha utekelezaji wa agizo hilo.