
Kiongozi wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Raila Odinga, amemkosoa vikali Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, kwa kutoa maagizo kwa maafisa wa polisi kuwapiga risasi hadi kufa watu wanaoshambulia vituo vyao.
Akizungumza katika ibada ya kanisa nyumbani kwake Bondo, Raila alilaani vikali matamshi ya Murkomen, akidai kwamba ni ukiukaji wa sheria waziwazi. Kwa mujibu wa Raila, amri hiyo haifai kikatiba, na inaweza kuharibu zaidi imani ya umma kwa vyombo vya usalama.
“Mtu yeyote anayetoa maagizo kwa polisi ampige risasi mtu yeyote anayekaribia kituo cha polisi, hiyo ni aibu kubwa. Aibu kwako,” alisema Raila.
“Hatupaswi kuhimiza kuondoa maisha ya mtu kwa njia isiyo ya kikatiba. Kama mtu ametenda kosa, mtu huyo anapaswa kupelekwa mbele ya sheria na kufikishwa mahakamani. Mahakama ikimpata na hatia, basi ahukumiwe," Raila alisema.
Alhamisi, muda mfupi baada ya kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu hali ya nchi kufuatia maandamano ya Gen Z, Murkomen alionekana kupendekeza kuwa polisi wanapaswa kutumia silaha zao iwapo watahisi wako hatarini wakiwa ndani ya kituo cha polisi.
Kufuatia ghadhabu ya umma, Murkomen alitoa ufafanuzi wa kauli hiyo, akisisitiza kuwa ilitafsiriwa nje ya muktadha wake na kwamba aliitoa kwa kuzingatia masharti ya kisheria.
“Kauli yangu ilitolewa kwa muktadha sahihi na kwa uelewa wa hali ya juu kwa misingi ya vifungu vya wazi vya sheria. Hakuna kiongozi, msomi, jaji, mwanahabari, mwanablogu, wala mchambuzi wa maoni ambaye amenipinga kisheria,” Murkomen alisema.
Maandamano ya Juni 25 yalikuwa na athari kubwa, huku mali ya thamani ya mamilioni ya shilingi ikiharibiwa, na watu kadhaa kupoteza maisha, baadhi yao kwa mikono ya polisi.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu pia yameripoti kuwa mamia ya raia kutoka mataifa mbalimbali walijeruhiwa vibaya katika vurugu za siku ya Jumatano.
Licha ya kumkosoa Murkomen, Raila pia aliwalaumu baadhi ya waandamanaji waliogeuza maandamano kuwa fursa ya kuharibu mali, katika siku iliyokusudiwa kuwa ya kuwaenzi vijana waliopoteza maisha yao wakati wa maandamano.
“Lakini wakati huo huo, tunalaani wahalifu waliotoka barabarani kuharibu mali na kuchoma kituo cha polisi. Huo si suluhisho,” Raila alitangaza.