
Aliyekuwa msemaji wa polisi Charles Owino amesema kuwa Boniface Kariuki, muuza bidhaa aliyepigwa risasi kichwani wakati wa maandamano ya kupinga ukatili wa polisi jijini Nairobi, alimtusi afisa wa polisi aliyefyatua risasi hiyo.
Ingawa alilaani tukio hilo la kupigwa risasi, Owino alisema Kariuki alitoa matusi yaliyomkera afisa huyo.
“Ilikuwa mazungumzo rahisi sana. Ukisikiliza kwa makini kipande cha video hicho utamsikia yule kijana akimtusi polisi. Lakini wewe ni afisa wa usalama, unapaswa kuwa na uvumilivu, na kama ni lazima upige, tumia risasi ya mpira. Unaona sasa athari yake kwa sura ya polisi kwa umma,” Owino alisema katika mahojiano na Citizen TV siku ya Jumatatu.
Afisa huyo, Klinzy Baraza Masinde, tayari amesimamishwa kazi na kufikishwa mahakamani pamoja na aliyekuwa mwenzake Duncan Kiprono, ambaye alikuwa naye wakati wa tukio hilo.
Owino pia alidai kuwa kutokana na umri wa afisa huyo aliyefyatua risasi, huenda hangeweza kudhibiti hasira zake.
“Kijana mdogo kama huyo ukimtukana bila shaka unajua kinachoweza kutokea,” alisema Owino.
“Polisi wamefunzwa vyema kuhusu mazingira yanayoruhusu matumizi ya silaha, na wanajua kuwa kila afisa huwa katika hali ambapo wanalazimika kufanya maamuzi peke yao bila kuwa na muda wa kushauriana na vitabu vyao au wakuu wao.”
Kariuki alitangazwa kuwa hana fahamu (brain dead) siku ya Jumapili, huku msemaji wa familia, Emily Wanjira, akisema kuwa madaktari katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta walithibitisha kuwa viungo vya Mwangi bado vinafanya kazi.
“Amebainika kuwa hana fahamu kabisa. Tunajua maana yake. Tunasubiri tu daktari atuthibitishie kuwa hayupo tena,” alisema.
Familia pia iliongeza kuwa bado kuna vipande zaidi vya risasi kwenye ubongo wake ambavyo havijatolewa.
Maafisa wawili wa polisi waliomshika Kariuki kwa nguvu kabla ya mmoja wao kumpiga risasi wanazuiliwa ili kuruhusu uchunguzi zaidi kufanywa na Mamlaka Huru ya Uangalizi wa Polisi (IPOA).