
Familia ya muuzaji barakoa, Boniface Mwangi Kariuki, inaamini kwamba huenda alifariki siku hiyo hiyo alipopigwa risasi na afisa wa polisi aliyepelekwa kudhibiti waandamanaji katika eneo la Biashara Kuu la Jiji la Nairobi majuma mawili yaliyopita.
“Tuna kila sababu ya kuamini kwamba Mwangi huenda alifariki siku hiyo hiyo alipopigwa risasi. Ni jambo la kusikitisha sana kwamba ilibidi azuiliwe kwa siku zote hizo hadi sasa ambapo tangazo linatolewa,” mshiriki wa familia alimwambia waandishi wa habari.
“Tuungane na kuiunga mkono familia. Nchi hii haielekei katika mwelekeo mzuri. Hatutaki kupoteza maisha. Tujiepushe na kupoteza maisha zaidi katika maandamano,” aliongeza.
Familia ilithibitisha Kariuki alifariki dunia Jumatatu saa 9:15 alasiri.
Kariuki,22, alipigwa risasi mnamo Juni 17 katika Barabara ya Tom Mboya jijini Nairobi wakati wa maandamano yaliyotaka Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Eliud Lagat ajiuzulu kufuatia kifo cha mtangazaji wa mitandaoni Albert Ojwang akiwa mikononi mwa polisi.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) siku ya Jumapili, msemaji wa familia Emily Wanjira alisema madaktari waliwataarifu kuwa shina la ubongo la Kariuki lilikuwa limekoma kufanya kazi, ingawa moyo wake bado ulikuwa unapiga kwa msaada wa mashine.
Video iliyosambaa sana mtandaoni ilionyesha maafisa wawili wa polisi wakimkabili Kariuki kabla ya mmoja wao kumpiga risasi kwa karibu na kumwacha bila fahamu.
Tangu wakati huo, Kariuki alikuwa amefanyiwa upasuaji mara tatu katika KNH, huku akihifadhiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).
Madaktari waliondoa kitu kama risasi kilichokuwa kimekwama kwenye ubongo wake, ambacho Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, Dkt William Sigilai, alisema huenda kilikuwa risasi ya mpira — ingawa uchunguzi wa kitaalamu bado unaendelea.
Vipande vya risasi vilipatikana kwenye ubongo wake, na alitegemea mashine kumsaidia kupumua.
Familia imesema bili ya hospitali sasa imevuka Shilingi milioni 3. Wameomba msaada kutoka kwa wahisani huku wakijiandaa kwa hali yoyote itakayofuata.
Katika hali iliyozidisha machungu yao, familia ilifichua kuwa walidanganywa Shilingi 200,000 na mtu aliyedai kuwasaidia kupanga matibabu.
Kisa cha kupigwa risasi kwa Kariuki kimezua hasira kote nchini, huku mashirika ya haki za binadamu yakitoa wito kwa polisi kuwajibishwa.
Amnesty International imemtaja Kariuki miongoni mwa waathiriwa wa ukatili wa polisi wakati wa maandamano yanayoongozwa na kizazi cha Gen Z, ambayo tayari yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 16 na wengine zaidi ya 400 kujeruhiwa kote nchini, wengi wao wakidaiwa kupigwa risasi na polisi.