
Taharuki imetanda Limuru baada ya Mratibu wa Vijana wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP), Peter Kawanjiru kutekwa nyara kutoka nyumbani kwake siku ya Jumatatu.
Mashuhuda walisema magari zaidi ya kumi, mengi yakiwa aina ya Subaru, yaliizingira nyumba yake huko Limuru.
Kundi la vijana waliokuwa na wasiwasi walikusanyika nje ya makazi hayo wakisihi kusitishwa kwa oparesheni hiyo.
Kawanjiru, ambaye ni mshirika wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, anadaiwa kutafutwa kuhusiana na maandamano ya kumbukumbu ya Juni 25 yaliyogeuka kuwa vurugu.
Anatuhumiwa kufadhili vitendo vya uharibifu na uchomaji wa mali katika maeneo ya Kiambu na Nairobi, ambapo miundombinu kadhaa ya serikali—ikiwemo Mahakama ya Kikuyu na vituo kadhaa vya polisi—iliteketezwa kwa moto.
Maandamano hayo yaligeuka kuwa ya hatari, ambapo vifo kadhaa viliripotiwa na watu zaidi ya 400, wakiwemo waandamanaji na maafisa wa polisi, walijeruhiwa.
Tukio hili limezidisha mvutano wa kisiasa, hasa miongoni mwa viongozi wa upinzani wanaolaani kile wanachokiita mwenendo unaokua wa utekaji nyara unaochochewa kisiasa.
Mwanasiasa Cate Waruguru alililaani tukio hilo kama ukiukaji wa haki za binadamu na ishara ya kuongezeka kwa utawala wa kiimla, akitaka Kawanjiru aachiliwe mara moja na kuwajibika kwa waliohusika na operesheni hiyo.
"Tunalani vikali utekaji nyara wa Mwenyekiti wa Kitaifa wa Vijana wa DCP, Wanjiku Thiga, kando ya Kamakis. Kitendo hiki cha woga na kisicho halali ni shambulio dhidi ya demokrasia, uongozi wa vijana na haki ya kutoa maoni tofauti," alisema.
"Tunataka aachiliwe mara moja na kwa usalama wake, utekaji nyara hauna nafasi katika jamii ya haki. Mwachilieni Kawanjiru, aliyetekwa jana katika shambulio lingine la wazi dhidi ya haki za binadamu. Tunaelekea wapi kama taifa ikiwa sauti zinazimwa kwa hofu badala ya hoja? Huu si uongozi, ni udikteta. Utekaji lazima ukome. Ukandamizaji lazima ukome. Tunataka haki, uwajibikaji na kuachiliwa mara moja kwa wote waliokamatwa kinyume cha sheria," aliongeza.
Kupotea kwa Kawanjiru kunajiri huku kukiwa na shinikizo linaloongezeka dhidi ya Gachagua, ambaye viongozi wa Kenya Kwanza wamemlaumu kwa kupanga machafuko hayo.
Hii ni licha ya Gachagua kuwa awali aliwahimiza Wakenya kuepuka maandamano hayo, akidai kuwa alikuwa na taarifa za kijasusi kwamba Rais William Ruto na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja walikuwa wameajiri wahuni wenye silaha ili kuwashambulia raia siku hiyo.
Tangu aondolewe madarakani, Gachagua amegeuka kuwa mmoja wa wakosoaji wakubwa wa Ruto, akijitokeza kama mtetezi mkubwa wa kuifanya urais wa Ruto kuwa wa muhula mmoja pekee.