
Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua alipigwa mawe akiwa katika eneo hilo akiendeleza kampeni ya kuwaunga mkono viongozi wa Muungano wa Upinzani wa Kitaifa kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika baada ya miaka miwili.
Gachagua alichapisha picha za sehemu ya msafara wake ulioharibiwa na watu wasiojulikana waliokuwa wamejihami kwa marungu, mawe na silaha nyingine hatari katika eneo la Chwele.
Kupitia taarifa rasmi, Gachagua alisema kuwa vurugu hazina nafasi katika taifa, na kwamba viongozi wanaotumia ukatili wanadhoofisha misingi ya utawala bora na demokrasia ya kweli.
“Watu wa Eneobunge la Kimilili katika Kaunti ya Bungoma wamezungumza kwa sauti kubwa na wazi: vurugu na mauaji ya kiholela hayana nafasi katika jamii yetu. Serikali zinazostawi kwa misingi ya ukatili hudumu kwa muda mfupi na hazina uhalali,” Gachagua alisema.
“Lazima tukemee vitendo kama hivyo popote vinapotokea na tusimame imara dhidi yake. Amani, haki na kuheshimu haki za binadamu ndizo nguzo za jamii yenye maendeleo,” aliongeza.
Akihutubia halaiki mnamo Ijumaa, Juni 4, 2025, katika mkutano wa hadhara Busia kama sehemu ya hitimisho la ziara ya Muungano wa Loyal Opposition Ukanda wa Magharibi, Gachagua aliwaambia wananchi kuwa jamii ya Waluhya “imekuwa ikidhulumiwa na kutupiliwa mbali mara kwa mara” na Raila kwa miongo kadhaa.
Aliukosoa vikali mtindo wa Raila wa kuingia serikalini kupitia siasa za handisheki baada ya uchaguzi, akisema kuwa kila mara anapoungana na serikali, wapiga kura wa eneo la Magharibi huachwa upinzani bila manufaa ya moja kwa moja.
Gachagua, ambaye kwa sasa ni kiongozi wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP), alisema kuwa eneo la Mlima Kenya pia limekumbwa na hali kama hiyo chini ya uongozi wa Rais William Ruto.
“Sisi wa Mlima Kenya pia tumetumika kisha kutupwa,” alisema. “Ruto alituahidi maendeleo lakini alituletea usaliti.”
Haya yanajiri siku moja tu baada ya Gachagua kudai kuwa ameweza kulinda eneo la Mlima Kenya dhidi ya ushawishi wa Rais Ruto, na kwamba yeye ndiye mwenye funguo.
“Nilikua naibu wa Ruto, je, mnamjua kuliko mimi? Je, mtatupa viongozi wenu ili tukubaliane namna ya kuchukua uongozi wa nchi hii? Huko Mlima Kenya nilimfungia Ruto nje, na funguo ninazo, nazibeba kila mahali ninaenda,” Gachagua alisema.