
Rais William Ruto ametetea kwa uthabiti ujenzi unaoendelea wa kanisa katika Ikulu ya Nairobi, akisema mradi huo unafadhiliwa kwa kutumia rasilimali zake binafsi na kwamba hana sababu ya kuomba msamaha kwa yeyote.
Akizungumza Alhamisi wakati alipokuwa mwenyeji wa viongozi kutoka Kaunti ya Embu wakiongozwa na Gavana Cecily Mbarire, Rais alithibitisha kujitolea kwake binafsi kwa imani ya dini na kupuuzilia mbali ukosoaji unaozunguka mpango huo.
"Mimi ni mtu naamini kwa Mungu, na sina samahani ya kuomba. Kwa kujenga kanisa, sina samahani, na hakuna mtu nitaomba msamaha," Ruto alisema.
Alithibitisha kuwa kanisa hilo linajengwa ndani ya maeneo ya Ikulu na alikiri kuwa ujenzi huo umevutia ufuatiliaji kutoka kwa vyombo vya habari.
"Naambiwa ati mpaka kwa gazeti leo kuna mtu anasema ninajenga kanisa hapa," alisema, akipuuza wasiwasi ulioibuliwa na vyombo vya habari.
Kauli za Rais zinajiri wakati mjadala wa umma unazidi kuongezeka kuhusu uhusiano kati ya dini na serikali, hasa kutokana na ujumbe wake wa mara kwa mara wa kidini na mahudhurio yake ya hafla za makanisa tangu alipoingia madarakani.
Hata hivyo, Ruto alisisitiza kuwa kujenga mahali pa ibada ndani ya makazi rasmi ya rais ni uamuzi wa kibinafsi na pia ni maonyesho ya imani yake.
Ujenzi wa kanisa hilo katika Ikulu unaendelea kama sehemu ya kile ambacho watu wa karibu na Rais wanakieleza kuwa ni tamanio lake la muda mrefu la kuwa na sehemu maalum ya ibada ndani ya Ikulu.
"Nimeamua nijenge kanisa inatoshana na State House na haitagarimu serikali ya Kenya peni moja. Nitajenga kwa sababu kanisa ya Mungu ni pahali inatoshana heshima," alisema Rais.
Kauli yake ilikuja baada ya ripoti katika sehemu ya vyombo vya habari kudai kuwa anajenga kanisa lenye thamani ya Shilingi bilioni 1.2 katika Ikulu.
Kwa mujibu wa chapisho hilo, hatua hiyo imeibua maswali kuhusu mgawanyo wa kikatiba kati ya dini na serikali.