logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Alai Apongeza Polisi kwa Kusimamia Maandamano ya Saba Saba kwa Ufanisi

Kupitia akaunti yake rasmi ya X, Jumatatu hiyo, Julai 7, 2025, Alai alieleza kuridhishwa kwake.

image
na Tony Mballa

Habari08 July 2025 - 09:39

Muhtasari


  • Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu ya Kenya (KNCHR) pia imethibitisha kuwa watu 10 walipoteza maisha yao wakati wa maandamano ya maadhimisho ya Siku ya Saba Saba.
  • Aidha, Tume hiyo imerekodi visa 29 vya majeruhi, matukio 2 ya utekaji nyara, na watu 37 waliokamatwa kuhusiana moja kwa moja na maandamano hayo.

Mwakilishi wa Wadi ya Kileleshwa katika Kaunti ya Nairobi, Robert Alai, amesifu Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) kwa jinsi walivyoendesha shughuli zao wakati wa maandamano ya Saba Saba yaliyofanyika Jumatatu, Julai 7, 2025.

Kupitia akaunti yake rasmi ya X, Jumatatu hiyo, Julai 7, 2025, Alai alieleza kuridhishwa kwake na namna maafisa wa usalama walivyoshughulikia maandamano hayo, ambayo yaliwaleta maelfu ya Wakenya barabarani kote nchini—wengi wao wakiwa vijana wa kizazi cha Gen Z—kusherehekea Siku ya Saba Saba.

“Huduma ya Polisi, SALUTE! Kazi nzuri sana leo. Mmeonyesha kuwa mna uwezo wa kulinda nchi kwa ufanisi. IMEVUTIA!” Alai aliandika.

Licha ya sifa hizo kutoka kwa Alai, NPS imethibitisha kuwa watu 11 walipoteza maisha yao katika maeneo mbalimbali ya nchi wakati wa maandamano hayo ya Saba Saba.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wa polisi, Muchiri Nyaga, NPS ilieleza kuwa wote 11 walikuwa raia wa kawaida, huku wengine 11 pia wakijeruhiwa.

Kulingana na taarifa hiyo, maafisa wa usalama 52 walijeruhiwa walipokuwa wakidhibiti hali wakati wa maadhimisho ya Siku ya Saba Saba.

Polisi pia walifichua kuwa Mbunge wa Manyatta, Gitonga Mukunji, alikamatwa. Hata hivyo, NPS haikutoa sababu ya kukamatwa kwake mara moja.

“Kwa masikitiko, taarifa za awali zinaonyesha kuwepo kwa vifo, majeruhi, uharibifu wa magari, na visa kadhaa vya uporaji kama ilivyoainishwa hapa chini. Aidha, washukiwa kadhaa wamekamatwa, wakiwemo Gitonga Mukunji, Mbunge wa Eneo Bunge la Manyatta,” sehemu ya taarifa ya NPS ilisoma.

Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu ya Kenya (KNCHR) pia imethibitisha kuwa watu 10 walipoteza maisha yao wakati wa maandamano ya maadhimisho ya Siku ya Saba Saba.

Aidha, Tume hiyo imerekodi visa 29 vya majeruhi, matukio 2 ya utekaji nyara, na watu 37 waliokamatwa kuhusiana moja kwa moja na maandamano hayo.

Katika taarifa yao rasmi iliyotolewa siku hiyo hiyo ya Jumatatu, Julai 7, 2025, Tume hiyo ilibainisha kuwa vizuizi vikubwa vya polisi viliwekwa kimkakati kwenye barabara kuu na maeneo ya kuingilia mijini, hasa jijini Nairobi, hali iliyosababisha usumbufu mkubwa kwa raia wa kawaida.

“Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu ya Kenya (KNCHR) inaendelea kufuatilia kwa karibu hali inavyoendelea wakati nchi inapoadhimisha Siku ya kihistoria ya Saba Saba. Kufikia saa 12:30 jioni leo, Tume ilikuwa imerekodi vifo kumi (10), majeruhi ishirini na tisa (29), na matukio mawili (2) ya utekaji nyara,” sehemu ya taarifa ya KNCHR ilisoma.

 

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved