
Askari wa magereza aliyekuwa ameunganishwa na kikosi cha kupambana na ghasia jijini Nairobi ili kudhibiti maandamano yaliyopangwa ya Saba Saba alivamiwa na kupokonywa bunduki yake aina ya G3 katika mtaa wa Majengo, Nairobi.
Afisa huyo, ambaye ni Sajenti Mkuu wa Magereza, alikuwa miongoni mwa makumi ya askari wa magereza waliokuwa wametumwa kusaidia polisi kudhibiti machafuko hayo.
Walifanikiwa kufunga njia za kuingia katikati mwa jiji, hali iliyosababisha machafuko kubaki katika maeneo ya pembezoni.
Afisa huyo alikuwa ametumwa katika mtaa wa Mombasa Ndogo, ndani ya eneo pana la Shauri Moyo jijini Nairobi, wakati tukio hilo lilipotokea.
Aliiambia polisi kwamba alikumbana na genge la watu waliomkimbiza kwa umbali mfupi kabla ya kuteleza na kuanguka huku wenzake wakimwacha.
Genge hilo lilimpokonya bunduki hiyo na kutoweka nayo kwenye mtaa huo.
Alisema bunduki hiyo ilikuwa na magazini yenye risasi 20 za moto na risasi 51 za mazoezi.
Wakati wa purukushani hizo, afisa huyo alipata majeraha katika mkono wa kushoto, bega la kushoto, nyonga ya kushoto na mguu wa kushoto.
Vitu vingine vilivyoibiwa wakati wa tukio hilo ni simu yake ya mkononi pamoja na kofia ya chuma ya maandamano.
Polisi walisema afisa huyo alipelekwa hospitalini akiwa katika hali ya wastani.
Tukio hilo lilichochea operesheni katika eneo hilo jioni, lakini haikufua dafu.
Wakazi wa eneo hilo walisema kulikuwa na maafisa wengi wa polisi waliotumwa katika juhudi za kuisaka bunduki hiyo.
Maandamano hayo yalifanyika katika angalau kaunti 17 nchini. Mali ya thamani isiyojulikana iliharibiwa wakati wa ghasia hizo.
Polisi walithibitisha Jumatatu kuwa watu 11 walifariki dunia kutokana na machafuko yaliyotokea wakati wa maandamano ya Saba Saba kote nchini. Polisi walisema maafisa wa polisi 52 walijeruhiwa, huku raia 114 wakipata majeraha wakati wa maandamano hayo.
Kulingana na taarifa ya polisi, magari ya polisi 125 yaliharibiwa, magari ya serikali 36 yaliharibiwa, huku magari ya raia 47 yakiharibiwa.
Polisi wamewakamata watu 567 waliokuwa wakishiriki maandamano hayo katika maeneo mbalimbali nchini.
Polisi waliwapongeza Wakenya kwa kutii sheria na kuitikia wito wa kudumisha amani na utulivu.
Hata hivyo, polisi waliongeza kuwa baadhi ya watu waliendelea kushiriki vitendo vya kihalifu, ikiwa ni pamoja na kuwashambulia maafisa wa usalama na kupora mali.
“Kwa masikitiko, ripoti za awali zinaonesha kuwepo kwa vifo, majeruhi, uharibifu wa magari na visa kadhaa vya uporaji,” ilisema taarifa ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi Jumatatu jioni.
Polisi walisema kila tukio lililoripotiwa litachunguzwa kwa kina kwa mujibu wa sheria.