
Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma amewataka Wakenya wamheshimu Rais William Ruto kama kiongozi wao.
Kaluma alikemea baadhi ya Wakenya kwa kuvuruga hali ya nchi na kufanya iwe vigumu kwa Rais kuendeleza maendeleo.
“Mheshimu Rais kama kiongozi wako na muunge mkono katika kujenga taifa. Amefanya maendeleo makubwa katika kuimarisha uchumi wa Kenya,” Kaluma alisema.
Aliwataka wale wanaoshiriki maandamano mitaani kusitisha mara moja, akionya kwamba mienendo yao inatishia kuwafukuza wawekezaji.
“Acheni maandamano ya mitaani; yanawafukuza wawekezaji. Kenya inahitaji nafasi za ajira kwa vijana wetu waliobobea, na hakuna anayewekeza katika mazingira ya sintofahamu na vurugu,” aliongeza.
Matamshi yake yanajiri siku moja baada ya nchi kushuhudia vurugu katika maadhimisho ya Siku ya Saba Saba yaliyofanyika Jumatatu.
Biashara kadhaa zilipata hasara kubwa kutokana na uporaji uliofanywa na vijana waliokuwa na hasira waliomiminika mitaani kupinga masuala mbalimbali, ikiwemo utekaji nyara na kupotezwa kwa nguvu kwa wenzao.
Jumla ya watu kumi waliuawa wakati wa maandamano ya Saba Saba yaliyofanyika Jumatatu, kwa mujibu wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KNCHR).
Tume hiyo ilisema kuwa ilibaini vifo kumi (10), majeruhi ishirini na tisa (29), visa viwili (2) vya utekaji nyara na watu thelathini na saba (37) kukamatwa katika kaunti kumi na saba (17) kufikia saa 12:30 jioni leo.
Tume hiyo ilieleza kuwa vizuizi vikubwa vya polisi viliwekwa katika barabara kuu na maeneo ya kuingia mijini, jambo ambalo lilitatiza kwa kiasi kikubwa usafiri wa watu, hasa katika jiji la Nairobi.
Vizuizi vya ziada viliripotiwa pia katika kaunti za Kiambu, Meru, Kisii, Nyeri, Nakuru na Embu.
“Raia wengi hawakuweza kufika kazini, licha ya agizo lililotolewa jana na Waziri wa Utumishi wa Umma, Geoffrey Ruku, akiitaka watumishi wote wa serikali kufika kazini bila kukosa,” KNCHR ilisema.
Biashara nyingi kote nchini zilibaki zimefungwa kutokana na hofu ya uporaji na uharibifu wa mali.
Matukio ya uporaji yaliripotiwa katika kaunti sita (6), na ofisi ya Hazina ya Maendeleo ya Maeneobunge ya Kerugoya Central ilichomwa moto na watu wanaoshukiwa kuwa wahalifu
Shughuli za masomo zilikwama kote nchini huku shule na taasisi nyingi za elimu zikiwa zimefungwa.
Tume ilipokea simu za dharura kutoka kwa wagonjwa waliokuwa hawana uwezo wa kufika katika vituo vya afya kutokana na kufungwa kwa barabara.
Mamia ya abiria walikwama kwenye vizuizi vya barabarani huku usafiri wa umma, ikiwemo wa anga na reli, ukitatizika pakubwa.
KNCHR imesema kuwa polisi wameendelea kupuuza agizo la Mahakama Kuu linalowataka maafisa wote wanaosimamia maandamano kuvaa sare rasmi na kuwa na vitambulisho wakati wote.
“Tume iliona maafisa wengi waliovaa kofia za kujificha nyuso, wakiwa hawajavaa sare, wakisafiri kwa magari yasiyo na alama maalum wakiwa doria katika kaunti za Nairobi, Kajiado na Nakuru.
“Pia, ilishuhudiwa uwepo wa magenge ya kihalifu yaliyojihami kwa silaha butu kama viboko, marungu, mapanga, mikuki, na pinde na mishale katika maeneo ya Nairobi, Kiambu, Kajiado na Eldoret. Katika Nairobi na Eldoret, magenge haya ya watu waliovaa kofia za kujificha nyuso yalionekana yakishirikiana na polisi,” KNCHR ilisema.