
Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, amewakashifu viongozi wa upinzani akisema hawana ajenda wala mpango wowote wa kuendeleza nchi, isipokuwa kushiriki siasa za mgawanyiko na chuki.
Akizungumza na wananchi katika Uwanja wa Mkunguni kwenye Kisiwa cha Lamu wakati wa hafla ya kuwawezesha wanawake kiuchumi siku ya Jumatatu, Wetang’ula aliwataka viongozi wa upinzani kuwasilisha mapendekezo ya jinsi ya kuendeleza taifa.
“Ni jambo la kusikitisha sana kuona viongozi wa upinzani hawana ajenda wala mpango. Ajenda ambazo wamezishikilia kila mara ni kama vile ‘Ruto Must Go’, ‘One Term’, ‘Kasongo’ na nyinginezo. Hatufikiri kuwa kuna manifesto kama hiyo duniani,” alisema Wetang’ula.
Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Kimani Ichung’wah, aliwaonya Wakenya kuwa viongozi wa upinzani hawana lolote la maana kwao. Aliwataka wakazi wa Lamu na Wakenya kwa ujumla kuwapuuza.
Alisisitiza kuwa aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, aliondolewa serikalini kwa kushindwa kuelewa ajenda halisi ya serikali ya Kenya Kwanza ambayo ni maendeleo kwa Wakenya wote, wakiwemo wa mashinani.
“Serikali ya Kenya Kwanza ni serikali jumuishi inayokusudia kuwawezesha wote. Ndiyo maana ilikumbatia mfumo wa kiuchumi wa odd bottom-up,” alisema Ichung’wah.
Naibu Rais Kithure Kindiki aliitaka nchi kujiepusha na maandamano na badala yake kutumia mazungumzo na mashauriano kutatua matatizo ya kitaifa.
Profesa Kindiki alisema nchi haiwezi kujengwa kupitia vurugu, uchochezi na ghasia.
Alisema licha ya wananchi kuwa na haki ya kikatiba ya kutoa maoni yao na kufanya maandamano, kila kitu kinapaswa kufanywa kwa amani na kwa kuheshimu sheria za nchi.
“Nawaomba ndugu zangu Wakenya. Hatuwezi kujenga nchi hii kwa vurugu, uchochezi au ghasia. Lazima tujifunze kutatua matatizo yetu ya kitaifa kupitia mashauriano, mijadala na njia za amani,” alisema Prof Kindiki.
Alipokuwa akihitimisha ziara yake ya wiki moja Pwani, Naibu Rais alisema maendeleo halisi yaliyotekelezwa kote nchini yameweka msingi imara wa muhula wa pili wa Rais William Ruto.
Naibu Rais alisema serikali inalenga kuhakikisha kila sehemu ya nchi inanufaika na ajenda ya maendeleo isiyo na ubaguzi, akiongeza kuwa hiki ndicho Wakenya wengi wanakitaka kutoka kwa serikali yoyote, na hivyo kumrahisishia Rais kupata muhula wa pili.
“Hatuzungumzi tu kuhusu mihula miwili. Tunasema kama tumefanya masoko ya kisasa 400 katika muhula wa kwanza, tutafanya masoko mengine 2,000 katika muhula wa pili. Kama tunajenga barabara kama hapa Lamu Mashariki ambako wamepata barabara ya kwanza ya lami, tutafanya zaidi katika muhula wa pili. Hatuwezi kusema sisi ni taifa lililoungana ikiwa kuna eneo ambalo halina hata barabara ya lami. Hiki ndicho Rais Ruto anabadilisha,” alisema Prof Kindiki.
Aliongeza kuwa Wakenya wote watapata miradi kwa usawa na mgao wa rasilimali, akisema jaribio lolote la kuwagawa kwa misingi ya eneo, kabila au dini litakataliwa.
Naibu Rais alisema ubaguzi uliokuwa ukihusishwa na utoaji wa vitambulisho katika kaunti za pembezoni umeondolewa na serikali ya Rais Ruto ili kuwezesha wakazi kupata hati hiyo muhimu bila vikwazo vingi.