
Kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, sasa anasema kuwa upinzani hauna nia yoyote ya mapinduzi ya kumpindua Rais William Ruto.
Kauli yake inajiri siku moja baada ya Rais Ruto kudai kuwa kuna njama kutoka kwa viongozi wa upinzani ya kutwaa mamlaka kwa njia zisizo za kikatiba.
Hata hivyo, akijibu madai hayo siku ya Alhamisi, Kalonzo alisema kuwa ingawa Wakenya wanatamani serikali mpya, hiyo si njia sahihi ya kufanikisha hilo.
Alisisitiza kuwa njia pekee wanayotaka Rais William Ruto aondoke uongozini ni kupitia uchaguzi.
“Wakenya hawataki kingine ila kwenda debe, kuiondoa serikali hii, kuweka serikali mpya itakayowasikiliza. Hakuna mtu anayetaka mapinduzi ya kiraia au jambo lolote kama hilo. Tunataka kumshinda William Ruto kwenye uchaguzi kwa kishindo,” alisema Kalonzo.
Ruto: Nitakabiliana Vikali na Wanasiasa Wanaochochea Ghasia
Wakati wa hafla iliyofanyika jijini Nairobi siku ya Jumatano, Rais Ruto alisema hataruhusu nchi kuvurugwa na watu wanaotaka mabadiliko ya uongozi kwa njia zisizozingatia Katiba.
Alipuuzilia mbali kile alichokitaja kuwa ni majaribio ya vikundi visivyo na subira vya kutaka kubadilisha uongozi mapema, akisema kuwa juhudi kama hizo hazitafaulu.
“Nchi hii haitaharibiwa na watu wachache wasio na subira wanaotaka mabadiliko ya serikali kwa kutumia njia zisizo za kikatiba. Hilo halitatokea,” alisema.
Ruto aliwataka wakosoaji wake kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2027 iwapo wanaamini wana sera bora kwa Wakenya.
“Ikiwa wana mipango, tukutane 2027. Waandae ilani yao ya uchaguzi, halafu tukutane mwaka huo. Hakuna njia ya mkato kati ya sasa na hapo,” alieleza.
Alisisitiza kuwa mabadiliko ya uongozi yanaweza kufanyika tu kupitia uchaguzi wa kidemokrasia, si kwa maandamano.
Karua Amtaka Ruto Ahakikishe Uchaguzi wa Haki 2027 la Sivyo Ang'atuliwe Mapema
“Nataka kuwaambia, hilo halitatokea. Na kama walikuwa wanafikiria hivyo, ni bora wafikirie upya,” alisema Ruto.
Mapema siku ya Jumatano, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua alikanusha madai kuwa upinzani unapanga kumpindua Rais Ruto mamlakani.
Akihutubia wanahabari saa moja baada ya hotuba ya Rais Ruto, Gachagua alisema kuwa vuguvugu la “Wantam” halina nia ya kuchukua mamlaka kwa njia zisizo halali.
“Tunataka kukushauri kuwa vuguvugu la Wantam halikulengi kukuondoa mamlakani nje ya Katiba,” alisema Gachagua.
“Mheshimiwa Rais, hakuna mtu anayetaka kuipindua serikali yako, hakuna mtu anayetaka uondoke madarakani kwa njia zisizo za kikatiba.”
Gachagua alisema kuwa upinzani, ambao umeshatangaza msimamo wake wazi, unalenga tu kumuondoa Ruto kutoka Ikulu kupitia debe mwaka 2027.