
Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua amepuuza pendekezo la kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga, la kuanzishwa kwa mazungumzo ya kitaifa ili kushughulikia changamoto zinazolikumba taifa.
Gachagua alisema kuwa Raila tayari amewahi kushiriki mazungumzo kama hayo hapo awali bila kuleta matokeo yoyote ya maana.
Wiki iliyopita, Odinga alikiri kuwa Wakenya wanapitia hali ngumu ya kiuchumi na ukiukaji wa haki za binadamu, na alipendekeza kuanzishwa kwa kile alichokiita “mkutano wa kitaifa” ili kuweka mwelekeo mpya kwa nchi kupitia ushirikishwaji wa wananchi na mageuzi.
Akizungumza na Wakenya wanaoishi Seattle, Jimbo la Washington, Gachagua alidai kuwa Raila ni mnafiki ambaye hutafuta kila nafasi ya kujiingiza serikalini kupitia mazungumzo.
Hata hivyo, alidai kuwa kila mara mambo yanapoharibika, Raila hujitenga na matatizo hayo.
“Raila hana umuhimu katika mazungumzo ya kisiasa kwa sababu kila uchaguzi hupoteza kisha hujipenyeza serikalini. Anataka kuwa serikalini lakini hataki kuwajibika. Yupo, lakini lawama huangukia mtu mwingine,” alisema Gachagua.
“Sasa anaona mambo yamekuwa magumu kwa Ruto; anajaribu kujitenga. Lakini kama angekuwa mzalendo wa kweli mwenye nia njema kwa nchi yetu, angejiondoa kabisa. Badala yake, anazungumza huku akiwa na mdomo uliojaa,” aliongeza.
Naibu Rais huyo wa zamani alisisitiza kuwa suluhisho la mwisho la kumuondoa Rais William Ruto madarakani ni kupitia Uchaguzi Mkuu wa 2027, akiwataka Wakenya kuwa na subira kwa miaka miwili ijayo.
Gachagua Sasa Atishia Kumpeleka Ruto ICC Kufuatia Amri ya Kuwapiga Risasi Waandamanaji
“Mazungumzo tunayohitaji ni ya debe mwaka 2027. Raila ameshiriki kila aina ya mazungumzo, lakini matatizo ya Kenya bado yako pale pale. Tunachohitaji ni uongozi wa mabadiliko. Ni wakati wetu kuvumilia kwa miaka miwili na kumaliza hili jambo moja kwa moja,” Gachagua alieleza.
“Wacha tukubali kuwa tuna tatizo na tusijaribu kulitatua kwa juujuu. Sidhani kama tatizo la Kenya linaweza kutatuliwa kwa kuzungumza na William Ruto. Hata yale mtakayokubaliana yatakuwa ni ya uongo, kwa hivyo hakuna cha kujadili naye kwa sababu haitafaulu.”
Pendekezo la Raila lilitolewa wakati taifa lilipokuwa likikumbuka miaka 35 tangu maandamano ya kihistoria ya Saba Saba, ambapo waandamanaji walikabiliana na polisi mitaani.
Wakati huo ulionyesha kuongezeka kwa hali ya kutoridhika miongoni mwa wananchi dhidi ya utawala wa Ruto kufuatia kupanda kwa gharama ya maisha na ukandamizaji wa polisi dhidi ya wakosoaji wa serikali na maandamano ya mitaani — ambayo mengi yamesababisha vifo na majeraha.