KK Mwenyewe, mchekeshaji aliyepata umaarufu kwa kuiga Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua, amefariki dunia.
Mchekeshaji huyo, ambaye jina lake kamili ni Zakaria Kariuki, alifariki usiku wa Jumatatu katika Hospitali ya Kiambu Level 4 baada ya kuugua kwa muda mfupi, kwa mujibu wa mchekeshaji mwenzake na mshirika wake wa kazi, Kafengo.
“Tunasikitika kutangaza kifo cha ghafla cha Zakaria Kariuki, maarufu kama Mr KK Mwenyewe. Alifariki jana jioni wakati akipokea matibabu katika Hospitali ya Kiambu Level 5,” Kafengo aliandika kupitia Facebook.
“Katika wakati huu wa huzuni, tunaomba msaada na maombi. Kwa familia na marafiki, Mungu atutie nguvu katika kipindi hiki kigumu. Roho yake ipumzike kwa amani.”
Ucheshi wa Kariuki wa kumwigiza Naibu Rais wa zamani ulimletea umaarufu mkubwa, ambapo alikusanya wafuasi milioni 1.1 kwenye TikTok na wengine 412,000 kwenye Facebook. Skit yake ya mwisho katika majukwaa hayo ilichapishwa tarehe 4 Julai.
Ucheshi wake wa moja kwa moja, mara nyingi ukioneshwa kupitia vipande vya video, uliwagusa Wakenya wengi kwani alijumuisha wahusika mbalimbali waliokuwa wa kawaida na wanaoeleweka kwa Mkenya wa kawaida.
Kuanzia kuiga wanasiasa, walimu hadi Wakenya wa kawaida, KK Mwenyewe alikuwa na hadhira ya kipekee kwa kila igizo fupi aliyochapisha, nyingi zikivutia maelfu hadi mamia ya maelfu ya watazamaji, hasa kupitia TikTok.
Wachekeshaji wenzake, mashabiki na hata wanasiasa walimiminika mitandaoni kuomboleza kifo chake, huku Seneta wa Busia Okiya Omtatah akimsifu kama mchekeshaji aliyekuwa na uwezo wa kutumia kejeli kuonyesha taswira ya jamii, si kwa kugawanya, bali kuamsha, kuelimisha na kuunganisha.
“Kenya imepoteza si tu mchekeshaji, bali mchambuzi wa kitamaduni na mzalendo kijana mwenye ujasiri. Pole zangu za dhati ziende kwa familia yake, marafiki na jumuiya nzima ya wasanii,” alisema Omtatah.
“Roho yake ipumzike kwa amani, na nuru yake iendelee kuwahamasisha waliobaki kwa ujasiri na ubunifu. Safari njema, Mr KK Mwenyewe.”
Gachagua, ambaye kuigwa kwake kulimpa Kariuki umaarufu mkubwa, alikuwa bado hajatoa tamko kuhusu kifo hicho kufikia wakati wa kuchapishwa kwa habari hii.
Ugonjwa uliosababisha kifo chake bado haujafichuliwa kwa umma, ingawa picha zake akiwa mgonjwa hospitalini zimesambaa sana mitandaoni.