
Nairobi, Kenya,, Julai 25, 2025 — Mbunge mteule Sabina Chege amempa hadhi ya juu kisiasa Naibu Rais Kithure Kindiki, akimtaja kama "kiongozi wa sasa wa Mlima Kenya" baada ya kile alichokitaja kama anguko la kisiasa la Rigathi Gachagua.
Katika mahojiano ya runinga ya ndani, Sabina alisema wazi kuwa enzi za uongozi wa kisiasa wa Mlima Kenya zimepitia mikononi mwa viongozi tofauti, lakini sasa zipo mikononi mwa Kindiki.
"Wakati Rais wa zamani alipokuwa madarakani, alikuwa kiongozi wa Mlima Kenya. Kisha tukawa na Rigathi kama kiongozi alipokuwa Naibu Rais, lakini baadaye akapokonywa mamlaka. Sasa tuna Kindiki kama kiongozi wa juu zaidi kutoka Mlima Kenya," alisema Sabina.
Gachagua Abaki Nje Ya Mchezo
Tangazo hili linajiri miezi kadhaa baada ya Gachagua kufurushwa kutoka wadhifa wa Naibu Rais, hatua iliyochochea hali ya sintofahamu kisiasa katika eneo la Mlima Kenya. Kwa sasa, Prof. Kindiki ndiye kiongozi wa juu serikalini kutoka eneo hilo.
"Siasa ni kuhusu nafasi na wakati. Kwa sasa, Kindiki ndiye kiongozi mwenye wadhifa mkubwa zaidi kutoka Mlima Kenya serikalini, jambo linalompa nafasi ya kuongoza eneo letu," alisisitiza Chege.
Kindiki Kama Chaguo La Maridhiano
Kwa miaka mingi, Kindiki amehusishwa na hulka ya utulivu, kuepuka siasa za mashambulizi na umakini wa kiutendaji. Wanaomchambua wanaona kuwa anaweza kuwa chaguo bora kwa kuleta mshikamano miongoni mwa wakazi wa Mlima Kenya.