
ADIS ABABA, ETHIOPIA, Julai 27, 2025 — Katika kile kinachoonekana kuwa hatua muhimu ya kidiplomasia, Rais William Ruto amewasili Ethiopia kuhudhuria Mkutano wa Pili wa Umoja wa Mataifa kuhusu Tathmini ya Mifumo ya Chakula (UNFSS+4), akibeba ujumbe mzito kuhusu mustakabali wa Afrika katika ajenda ya chakula na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mara nyingine, Kenya imesikika katika majukwaa ya kimataifa – si kwa siasa za ndani, bali kwa sauti yake katika ajenda ya maendeleo endelevu na usalama wa chakula.
Rais Ruto ametua mjini Addis Ababa, Ethiopia, akiwa na ujumbe wa matumaini na mageuzi kwa Afrika nzima.
Akiwasili, Rais Ruto alipokelewa na Naibu Waziri Mkuu wa Ethiopia, Temesgen Tiruneh, katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bole, ishara ya mapokezi ya hadhi ya juu kwa kiongozi wa taifa jirani.
Katika hotuba yake inayotarajiwa kuwasilishwa rasmi kwenye mkutano huo, Rais Ruto anatarajiwa kutoa msimamo wa Kenya kuhusu umuhimu wa kubadili mifumo ya chakula kwa mujibu wa mahitaji ya mabadiliko ya tabianchi, ukuaji wa idadi ya watu na changamoto za kiuchumi duniani.
Msemaji wa Ikulu ya Nairobi, Hussein Mohamed, alieleza kuwa Rais Ruto pia atashiriki mikutano ya pande mbili na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni na Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahamoud Ali Youssouf.
"Ajenda ya Kenya itahusu usalama wa chakula, ushirikiano wa kikanda, biashara, miundombinu na diplomasia ya kimataifa," alisema Hussein.
Mkutano wa UNFSS+4 unajumuisha viongozi kutoka mataifa mbalimbali, washirika wa maendeleo na sekta binafsi, wote kwa pamoja wakijadiliana namna ya kuharakisha utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu kupitia mifumo thabiti ya chakula.