
NAIROBI, KENYA, Julai 29, 2025 — Katika ujumbe uliojaa hisia na msimamo dhabiti, binti wa Rais William Ruto, Charlene Ruto, amewaambia Wakenya kuwa ni lazima kuweka mipaka kati ya uanaharakati wa kweli na tabia hatari za mitandaoni kama matusi, kudhalilisha watu, kueneza chuki, na kile alichokiita “utamaduni wa kufuta watu”.
Charlene alisema kuwa mitandao ya kijamii imegeuka kuwa uwanja wa mashambulizi ya kihisia badala ya kuwa jukwaa la kujenga jamii yenye maadili na mshikamano.
“Ni wakati wa kuweka upya utamaduni wetu wa kidijitali. Kutusi, kudhalilisha, mashambulizi ya mtandaoni na kampeni za kufuta watu si uanaharakati – bali ni aina ya ukatili,” alisema Charlene kupitia ujumbe alioutuma kwa umma.
Madhara ya Kisaikolojia
Charlene alisisitiza kuwa matamshi mabaya na kampeni za chuki zina madhara makubwa kwa wahusika, hasa kwa afya ya akili.
“Madhara ya kihisia na kisaikolojia yanayosababishwa na tabia hizi ni ya kweli, na tunapaswa kuyachukulia kwa uzito mkubwa,” aliongeza.
Wadau wa afya ya akili wamekuwa wakionya kuhusu ongezeko la matatizo ya kisaikolojia kutokana na ukatili wa mitandaoni. Kwa mujibu wa utafiti, idadi ya vijana wanaopata msongo wa mawazo, kujitenga kijamii na hata kujiua imeongezeka kwa kasi, hasa miongoni mwa wale wanaoshiriki katika mijadala ya mtandaoni.
Simama kwa Haki, Siyo Chuki
Charlene aliwahimiza wanamtandao, hasa kizazi cha vijana, kutumia majukwaa ya kidijitali kwa ujenzi wa hoja, elimu na kusaidia jamii badala ya kuwadhuru watu.
“Kukosoa ni haki, lakini tunapaswa kufanya hivyo kwa heshima na hoja. Tusikubali maumivu ya wengine kuwa burudani yetu,” alisema kwa msisitizo.
Akaongeza kuwa tofauti ya maoni haipaswi kuwa chanzo cha uhasama, bali njia ya kukuza mijadala yenye maana.
Wito wa Mageuzi ya Kidijitali
Wito wa Charlene umeibua mjadala mpana kuhusu uhuru wa kujieleza, mipaka ya maadili na dhima ya majukwaa ya mitandaoni katika kujenga taifa lenye ustaarabu wa kidijitali.
“Tunaweza kuwa na mitandao yenye maudhui makali lakini yenye heshima. Mageuzi haya yanahitaji sisi wote,” alihitimisha.