
KAMPALA, UGANDA, Jumanne, Novemba 11, 2025 – Rais Yoweri Museveni ameonya Uganda inaweza kuchukua hatua kali dhidi ya Kenya, akisema kunyimwa Bahari ya Hindi kunatishia uchumi, usalama na hadhi ya taifa lake.
Museveni alisema Uganda inaendelea kupoteza nguvu za kibiashara na kiusalama kwa sababu haina ufikiaji wa bahari, jambo alilosema halina haki wala mantiki kwa taifa linalotegemea masoko ya nje.
“Tunaumia kiuchumi. Tumefungwa na mipaka ambayo haina kueleweka kwa kizazi chetu,” alisema.
Alitamka hayo wakati wa kipindi cha mazungumzo cha redio katika Nyumba ya Wageni ya Mbale.
Museveni Ataja Hasara Kubwa Za Kukosa Bahari
Akiingia katika maelezo ya kina, Museveni alisema Uganda inashindwa kutekeleza majukumu ya msingi ya kiusalama kutokana na ukosefu wa maji ya bahari.
Hapa ndipo alitoa kauli yake ndefu, sasa kwa Kiswahili sanifu:
“Hapa Uganda, hata kama tungetaka kujenga jeshi la majini, tutajengaje? Hatuna ufikiaji wa bahari. Mpangilio wa kisiasa barani Afrika hauna mantiki kabisa. Baadhi ya nchi hazina bahari si kwa sababu za kiuchumi tu bali pia kwa sababu za ulinzi. Unakuwa umekwama. Nitauzaje bidhaa zangu nje?
“Ndiyo maana tumekuwa na mazungumzo yasiyoisha na Kenya. Yakisimama hapa, yanaibuka mengine. Reli, bomba la mafuta — tunajadili tu. Lakini ile bahari ni yangu. Kwa sababu ni bahari yangu. Nina haki juu ya bahari hiyo. Na huko mbele, tunaweza kuwa na vita,” Museveni amesema.
Mazungumzo Na Kenya Yamekwama Kwa Muda Mrefu
Museveni alisema mazungumzo kati ya Uganda na Kenya kuhusu miradi ya reli, bomba la mafuta na usafirishaji wa bidhaa yamekuwa yakirudiarudia bila hatua thabiti. Alisema Uganda imekuwa “ikingoja bila mwisho,” jambo ambalo limeleta ukakasi kwa upande wa Kampala.
Kwa miaka mingi, Uganda imekuwa ikilalamika juu ya gharama kubwa na ucheleweshaji wa mizigo katika Bandari ya Mombasa.
Museveni ameonyesha kukerwa na urasimu wa mara kwa mara unaokwamisha bidhaa zake kufika sokoni kwa wakati.
Amesema Uganda imewahi kuangalia uwezekano wa kuhamisha shughuli zake kwenda Tanzania ikiwa mambo hayatabadilika.
Wachambuzi Watoa Tahadhari Kuhusu Athari Za Kauli Hii
Wachambuzi wa siasa za kikanda wanasema kauli ya Museveni inaweza kuchochea mgogoro mpya ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Wanasema suala la bahari linaweza kuathiri uhusiano wa kibiashara, usalama wa pamoja na mipango ya miundombinu inayotegemea ushirikiano wa nchi hizo.
Mtu mmoja aliyefuatilia masuala ya EAC alisema: “Kauli hii ina uzito mkubwa. Inaonyesha ukosefu wa uaminifu na kuhitaji mabadiliko ya haraka.”
Kenya Yanyamaza Ikisubiri Mwelekeo Mpya
Serikali ya Kenya haijatoa tamko rasmi kufuatia matamshi ya Museveni.
Afisa mmoja katika Nairobi alisema bila kutajwa jina kuwa Kenya “haiendi kinyume na maslahi ya Uganda” na inachokifanya ni kukamilisha mambo ya kiufundi.
Museveni Atoa Wito Wa Mapinduzi Ya Mipaka Ya Afrika
Museveni alisema kuwa mipaka iliyowekwa enzi za ukoloni imeacha baadhi ya mataifa bila bahari, hali aliyoitaja kuwa “kikwazo cha maendeleo.”
“Afrika haiwezi kuendelea kukosa mpangilio wa haki. Baadhi ya mataifa yana bahari tatu, mengine hayana hata tone. Hili halina mantiki,” alisema.
Bahari Ya Hindi Yazidi Kuleta Mvutano Mpya
Kauli ya Museveni imeweka presha mpya kwa Kenya na Uganda, huku wadadisi wakisema lazima kuwe na majadiliano mapya kuhusu masuala ya bahari, usalama na biashara ili kuepusha mgogoro mkubwa unaoweza kuzuka.
Kwa sasa, macho ya eneo lote yako kwa Kampala na Nairobi, kusubiri hatua zitakazofuata baada ya kauli hii nzito ya rais wa Uganda.








© Radio Jambo 2024. All rights reserved