
Seneta wa Kaunti ya Vihiga, Geoffrey Osotsi, amesema jamii ya Waluhya haina mpango wa kuondoka katika chama cha ODM.
Akizungumza katika Kaunti ya Vihiga, Osotsi alipuuza vikali madai kwamba Waluhya wanatafuta mwelekeo mpya wa kisiasa, akisema tofauti zozote ndani ya ODM zitashughulikiwa kwa njia ya mazungumzo ya ndani.
“Kama ni kugombana, tutagombana ndani ya chama. Hatuendi mahali hadi tusikizane,” alisema Osotsi.
Kauli yake inakuja wakati ambapo baadhi ya wachambuzi wa siasa wanahoji iwapo ODM itaendelea kushikilia maeneo yake ya jadi ya uungwaji mkono bila ushawishi wa moja kwa moja wa Raila Odinga, ambaye kwa miongo kadhaa amekuwa nguzo kuu ya chama hicho.
Waluhya na uhusiano wao na ODM
Jamii ya Waluhya imekuwa miongoni mwa nguzo muhimu za ODM tangu chama hicho kilipoanzishwa. Kwa mujibu wa Osotsi, uhusiano huo haukujengwa kwa bahati, bali kwa juhudi za muda mrefu.
“Nimesikia wengine wakisema Waluhya wanataka kutoka ODM. Tutoke ODM tuachie nani?” aliuliza.
Alisema Raila Odinga alifanya kazi kubwa kujenga uaminifu na heshima na jamii ya Waluhya, jambo lililowafanya kumuunga mkono kwa dhati katika chaguzi kadhaa zilizopita.
Ushauri na maridhiano ndani ya chama
Osotsi alisisitiza umuhimu wa mashauriano ya kina ndani ya ODM, akisema kuwa mustakabali wa chama hicho lazima ujadiliwe kwa kuwashirikisha wanachama wote wakuu.
“Tunahitaji mashauriano.Maeneo yote yanayoiunga mkono ODM, ikiwemo eneo la Waluhya, lazima yashirikishwe ipasavyo,” alisema.
Kwa mujibu wake, Waluhya lazima wawe sehemu ya maamuzi yatakayofanywa kuhusu mwelekeo wa chama katika siku zijazo.
Kwa nini kura za Waluhya si rahisi kuhamishwa
Seneta huyo alionya dhidi ya dhana kwamba kura za Waluhya zinaweza kuhamishwa kwa urahisi kwenda kwa chama au kiongozi mwingine.
“Waluhya walimuunga mkono Raila kwa sababu alifanya kazi kwa bidii kupata heshima yao,” alisema.
Aliongeza kuwa uungwaji mkono huo ulijengwa kwa muda mrefu na hauwezi kuhamishwa kwa urahisi bila juhudi mpya.
“Kuna mtu lazima aje afanye kazi kwa bidii zaidi, awashirikishe Waluhya, awe rafiki yao, ndipo apate uungwaji mkono wao,” aliongeza.
ODM na changamoto za kipindi kijacho
Kauli ya Osotsi inaonekana kulenga kuimarisha mshikamano ndani ya ODM huku chama hicho kikikabiliwa na maswali kuhusu uongozi, umoja na mvuto wake wa kitaifa.
Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa kauli kama hizi ni muhimu katika kudumisha utulivu wa kisiasa katika maeneo ambayo yamekuwa ngome za chama hicho kwa miaka mingi.
Kwa sasa, ujumbe wa Seneta Geoffrey Osotsi uko wazi. Jamii ya Waluhya bado iko ndani ya ODM, na haina mpango wa kuondoka.
Kwa chama hicho, changamoto iliyopo si kuhofia kuhama kwa wafuasi wake, bali kuhakikisha mashauriano, ushirikishwaji na uongozi thabiti katika kipindi kijacho cha siasa za Kenya.



© Radio Jambo 2024. All rights reserved