RIP! Babake Jahmby Koikai adaiwa kufariki dunia wakati bintiye akizikwa

Kifo cha Bw Koikai kinajiri siku moja tu baada ya yeye kumuomba msamaha bintiye marehemu hadharani.

Muhtasari

•Bw Koikai alifariki siku ya Ijumaa asubuhi, siku ambayo mwili wa binti yake ulizikwa katika Makaburi ya Lang’ata, kaunti ya Nairobi.

•Alikuwa amekiri kwamba hakuwa baba bora kwake wakati wote na kwamba alimuangusha wakati alipomhitaji zaidi.

amefariki dunia baada ya binti yake Njambi kuzikwa.
Bw Daniel Koikai amefariki dunia baada ya binti yake Njambi kuzikwa.
Image: HISANI

Bw Daniel Koikai, baba ya marehemu mtangazaji wa reggae Mary Njambi almaarufu Fyah Mummah Jahmby amedaiwa pia amefariki.

Duru za kuaminika zinasema kuwa Bw Koikai alifariki siku ya Ijumaa asubuhi, katika hali isiyoeleweka.

Mzee huyo alifariki mnamo siku ambayo mwili wa binti yake ulikuwa ukizikwa katika Makaburi ya Lang’ata, kaunti ya Nairobi. Marehemu hakuwepo wakati wa mazishi ya bintiye..

Mwili wa marehemu Bw Koikai unaripotiwa kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Montezuma Monalisa.

Kifo cha Bw Koikai kinajiri siku moja tu baada ya yeye kumuomba msamaha bintiye marehemu hadharani. Alikuwa amekiri kwamba hakuwa baba bora kwake wakati wote na kwamba alimuangusha wakati alipomhitaji zaidi.

Katika ujumbe kwa bintiye ulionakiliwa katika ratiba ya ibada ya ukumbusho iliyofika Radio Jambo, Bw. Koikai alifunguka kuhusu kumbukumbu nzuri na mbaya zake yeye na bintiye.

Alikiri kwamba anajilaumu sana kwa nyakati ambazo hawakuwa na maelewano mazuri, akibainisha kuwa alikosa nafasi za kurekebisha mambo kati yao.

"Wakati nyakati zilikuwa mbaya, tulikuwa tukienda kwa siku na miezi bila kuzungumza, jambo ambalo najilaumu na nitafanya kila wakati kwani nilipoteza nafasi ya kurekebisha mambo na wewe. Siku zote zitalemea sana moyo wangu,” alisema.

Katika ujumbe wake, Bw Koikai alikiri kwamba hakuwa baba bora kwa bintiye kila mara.

Alizungumza kuhusu kutokuwepo  katika maisha ya bintiye na kumwachia mzigo wa kumlea kwa mzazi mwenzake, na pia kutokuwepo kwa ajili yake wakati ambapo alikuwa akimhitaji zaidi.

"Ninakiri sikuwa baba mzuri na bora wakati wote kwako, na nilimwachia mama yako mzigo kwa hili. Matukio ambayo nilishindwa kwa njia nyingi kusimama nawe ulipokuwa ukipambana na ugonjwa wa endometriosis, najuta sana. Nimechelewa sana kujuta. Ninaweza tu kuishi na ukweli kwamba nilikuangusha wakati ulinihitaji sana, na sijivunii hata kidogo kwa mwenendo wangu,” alisema.

Pia alifunguka kuhusu uhusiano wao ambao aliutaja kuwa mzuri na mbaya katika nyakati fulani.

“Kuhusu uhusiano wetu, tulikuwa na nyakati nzuri na mbaya. Nyakati zilipokuwa nzuri, tungeenda kununua bidhaa na kula chakula cha mchana katika baadhi ya mikahawa mjini, na ulifurahia mikutano hiyo kikamilifu. Nina’miss sana nyakati nzuri tulizoshiriki pamoja,” Bw Koikai alisema.

Siku ya Alhamisi, Juni 13, familia na marafiki wa marehemu Njambi walifanya ibada ya ukumbusho ya marehemu mtangazaji huyo wa reggae katika Nairobi Chapel, iliyo kwenye Barabara ya Ngong. Marehemu Bw Koikai alikuwepo.