Ni Pigo kwa Rigathi Gachagua baada ya jopo la majaji watatu wa mahakama kuu kuondoa mari ya kuzuia kuapishwa kwa naibu wa rais mpya mteule, Abraham Kithure Kindiki.
Jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Eric Ogola pia linajumuisha Jaji Anthony Mrima na Fredah Mugambi.
"Suala hili lina maslahi makubwa ya umma, na tunasalia kujitolea katika uchunguzi wa haraka wa malalamiko," Ogola aliamua.
"Maagizo ya kihafidhina yaliyotolewa Oktoba 18 katika Mahakama Kuu ya Kerugoya yameondolewa au kutengwa."
Mahakama Kuu ya Kerugoya imetoa maagizo ya kumzuia Kithure Kindiki kushika wadhifa wa Naibu Rais kusubiri kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi iliyowasilishwa mbele yake.
David Munyi Mathenge na Peter Gichobi Kamotho walitaka maagizo hayo baada ya Bunge la Kitaifa kuidhinisha uteuzi wa Kindiki kama Naibu Rais mpya, siku moja baada ya Seneti kupiga kura ya kumtimua Rigathi Gachagua.
Mathenge na Kamotho wameshtaki Seneti, Spika wa Seneti na wengine wawili. Kesi hiyo iliwasilishwa chini ya cheti cha dharura mbele ya Jaji Mwongo Richard Mururu.
Kesi hiyo baadaye iliunganishwa na nyingine zilizokuwa zimewasilishwa Nairobi.