Polisi wamzuilia mwanamume kwa madai ya kumuua mkewe, Embu

Muhtasari

  • Mshukiwa ametambulika kama Martin Mugendi.

  • Kulingana na DCI, majirani walianza kushuku kitu baada ya kukosa kumuona marehemu.

crime scene
crime scene

Maafisa wa DCI katika wa Embu wanachunguza kisa wanachoshuku kuwa cha mauaji ambapo mwanamume mmoja anaaminika kumuua mkewe mwenye umri wa miaka 34 siku ya Jumanne, kabla ya kuweka barua feki ya kujiua karibu na mti ulipopatikana mwili.

Kulingana na taarifa ya DCI siku ya Jumatano, mwili ambao ulikuwa umefungwa kwa kamba na kutegwa mtini katika hali ya kuketi ulipatikana takriban mita 500 kutoka nyumbani kwa marehemu.

Mshukiwa ametambulika kama Martin Mugendi.

"Uchunguzi wa awali wa maafisa wa upelelezi wa DCI ulibaini kuwa marehemu alikuwa amekula chakula cha jioni na mumewe (mtuhumiwa) karibu saa tatu jioni Jumanne, muda mfupi kabla ya kumgeukia kwa makofi na mateke," maafisa wa DCI walisema.

Huku akijifanya kuwa kila kitu kilikuwa shwari mshukiwa anasemekana kumpeleka bintiye kwa nyumba ya jirani siku ya Jumatano asubuhi kabla ya kuelekea kazini.

Kulingana na DCI, majirani walianza kushuku kitu baada ya kukosa kumuona marehemu akiendeleza shughuli zake kama alivyozoea.

Walishangazwa pia kwamba bwanake hakuwa anasema kitu kuhusu alikokuwa mkewe na kupelekea wao kuanza zoezi la kumsaka.

Mwili wake ulipatikana na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti na unasubiri kufanyiwa upasuaji kubaini kilisababisha kifo cha marehemu.

Mshukiwa ataendelea kusalia korokoroni huku wachunguzi wakipekuwa pekua kutegua kitendawili cha kifo cha mama huyo.