Jamaa azuiliwa baada ya simu yake iliyopotea kutumika katika uhalifu

Hakimu mkuu mwandamizi Monica Maroro (Kulia)
Hakimu mkuu mwandamizi Monica Maroro (Kulia)
Image: CLAUSE MASIKA

Mwanamume ambaye anasemekana kupoteza laini yake ya Safaricom na kisha ikatumiwa kutekeleza uhalifu amezuiliwa kwa siku saba akisubiri uchunguzi wa polisi kuhusu tukio hilo.

Hakimu mkuu mwandamizi wa Kibera Monica Mororo aliagiza kwamba Michael Kamau Kaniaru azuiliwe baada ya kuruhusu ombi la polisi.

Katika ombi hilo polisi waliambia mahakama kwamba nambari ya mshukiwa ilikuwa imetumika sana kuwasiliana na watekaji nyara hatua inayomhusisha na uhalifu huo.

 

"Baada ya kutafuta haraka, simu ya rununu inayodhaniwa kuwa ya watekaji nyara iliyopatikana kwenye kiti cha dereva mwenza na uchambuzi wa simu iliyopatikana kwenye lori ulifichua mawasiliano ya kila mara kati ya mshtakiwa na nambari ya simu iliyopatikana," aliambia korti.

Afisa huyo alisema kwamba mshtakiwa alikamatwa Januari 11 katika mtaa wa Pipeline siku kadhaa baada ya tukio hilo kutendeka.

"Mnamo Novemba 19, 2020, mlalamishi katika kesi hii Zheng Hong distillers kupitia mkurugenzi wao aliripoti kwamba moja ya malori yao, yenye nambari ya usajili KCX 815K ilikuwa imebadilishwa mkondo na ilikuwa nje ya njia ya kawaida," aliambia korti.

Alisema kwamba dereva wa lori hilo alikuwa katika barabara ya Waiyaki ambapo alikuwa ameenda kupeleka bidhaa za kampuni hiyo.

"Katika eneo la Zambezi, alisimamishwa na gari aina ya Toyota Fielder nyeupe ambayo ilikuwa na watu watano waliokuwa wamejihami kwa bastola, walimweleza kuwa ujumbe ulikuwa umesambazwa kwamba gari hilo lilikuwa limeibwa na wakamwamuru awekwe ndani ya gari ambamo alilala akiwa amefunikwa uso na baadaye kumtupa mahali pasipojulikana, "aliongeza.

Maafisa wa upelelezi waliambia mahakama kwamba dereva huyo baadaye aliokolewa na kusafirishwa hadi kituo cha polisi cha Athi River kuripoti kisa hicho.

Mahakama iliambiwa kwamba lori hilo lilikuwa na kifaa cha kulifuatilia ambacho kilisaidia sana katika kukamatwa kwa washukiwa.

 

Kesi hiyo itaendelea Januari 18.