Mwalimu mkuu aponea kifo, mwanafunzi amshambulia kwa panga

Muhtasari

  • Mwanafunzi aliingia katika ofisi ya mwalimu mkuu akiwa amebeba panga.

  • Mwalimu mkuu aliokolewa na walimu na wafanyikazi wa shule waliomzidi nguvu mshukiwa.

Mwanafunzi aliyejaribu kumshambulia mwalimu mkuu kwa panga
Mwanafunzi aliyejaribu kumshambulia mwalimu mkuu kwa panga
Image: HISANI

Siku moja tu baada ya mwanafunzi mmoja kuwajeruhi walimu wake wawili katika shule moja kaunti ya Kisii, Siku ya Jumatano mwanafunzi mwingine alikamatwa baada ya kudaiwa kujaribu kumkata kwa panga mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Mokwerero eneo la Kitutu Masaba.

Mwanafunzi huyo kidato cha pili anasemekana kuingia katika ofisi ya mwalimu mkuu akiwa amejihami kwa panga aliyokuwa ameibebea ndani ya begi lake la vitabu.

Kulingana na mwalimu mmoja katika shule hiyo, mwalimu mkuu aliokolewa na walimu wengine wakishirikiana na wafanyikazi wa shule hiyo  baada ya kupiga kamza waliomzidi nguvu mwanafunzi huyo wa kiume kabla ya kuita polisi.

 

Siku ya Jumatatu mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya Kisii aliwajeruhi walimu wawili kwa kisu baada ya mwalimu mmoja kujaribu kumuadhibu kwa kufika shuleni akiwa amechelewa.

Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 17 siku ya Jumanne alikanusha mashtaka ya kujaribu kuua walimu wake wawili katika shule hiyo.

Mwanafunzi huyo alikanusha mashtaka hayo mbele ya hakimu Mkaazi Mwandamizi Onchoro wakati aliposhtakiwa katika mahakama ya Kisii.

SRM Onchoro alimwachilia mshukiwa kwa dhamana ya Shilingi 100,000 na mdhamini wa kiasi sawa au dhamana ya pesa taslimu ya Shilingi 50, 000 au kupelekwa rumande ya watoto ya Manga Kaunti ya Nyamira kwasababu alikuwa mwanafunzi.